Friday, November 10, 2017

CCM KUENDELEA KUSIMAMIA UTOLEWAJI WA FURSA ZAIDI KWA MAKUNDI NA WATU WENYE ULEMAVU NCHI

Novemba 10, 2017

Katika semina ya uwezeshaji na maendeleo kwa wanawake wenye ulemavu iliyofanyika Makao Makuu ya SHIVYAWATA Mkoa wa Dar Es Salaam, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehimiza serikali kuendelea kuwezesha makundi yote maalumu yenye uhitaji hususani kundi la watu wenye ulemavu.

Semina hiyo iliyoratibiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ilihudhuriwa na  Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Bi. Ummy Hamisi Nderiananga, Maafisa kutoka Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)- Lumumba Idara ya Itikadi na Uenezi Ndg. Shabani Shabani na Ndg. Saidi Saidi, Maafisa kutoka Halmashauri za Manispaa ya Ilala na Temeke, Wataalamu wa uandishi wa maandiko ya miradi na biashara na washiriki wa semina hiyo ambao ni wanawake 110 wenye ulemavu wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali Jijini Dar Es Salaam.

Maafisa kutoka Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametoa rai ya kutowanyanyapaa watu wenye ulemavu na  kusisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu na kuwapatia kipaumbele na fursa mbalimbali za kimaendeleo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 fungu la 57,  58 na 63.

Hivi karibuni CCM iliutangazia umma juu ya dhamira yake ya kuwasaidia wanafunzi ambao ni yatima, wenye ulemavu ama wenye wazazi wenye ulemavu wanaojiunga ama wanaendelea na masomo ya Chuo Kikuu kupata Mikopo ya elimu ya juu. Zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa sana.

Huu ni muendelezo wa usimamizi na ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani kwa vitendo na kuhuisha na kuhamasisha kauli mbiu ya CCM MPYA TANZANIA MPYA na kuwa “Chama cha wanachama na kinachoshughulika na shida za watu”.

Imetolewa Na;

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI.
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM).

No comments:

Post a Comment