Sunday, October 1, 2017

300 watibiwa maradhi ya moyo JKCI kila siku

WAKATI dunia i k i a d h i m i s h a Siku ya Moyo Duniani, Tanzania ina kila sababu ya kusherehekea maadhimisho hayo kifua mbele kutokana na mapinduzi yanayoendelea kufanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Dar es Salaam katika kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kutokana na magonjwa ya moyo.

Umuhimu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, unatokana na athari kubwa zinazotokana na magonjwa ya moyo nchini Tanzania, Afrika na Duniani kote kutokana na data za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka huu, kuonesha kuwa magonjwa ya moyo ndio magonjwa hatari zaidi duniani hivi sasa na ndiyo yanayoua watu wengi zaidi.

Data za hivi karibuni za WHO zinaonesha kuwa watu takribani milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, yakifuatia magonjwa ya saratani yanayoua watu takribani milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanaua watu milioni nne na kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka. Tafiti zinaonesha pia kuwa zaidi ya watu milioni 75 huugua magonjwa hayo ya moyo kila mwaka duniani.

Ingawa daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya JKCI, Tulizo Sanga, anasema Tanzania haijafanya utafiti wa kina wa kubaini ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo katika siku za hivi karibuni, lakini takwimu za WHO za mwaka 2011, zilionesha kuwa katika kila wagonjwa 100,000 waliokuwa na matatizo ya moyo 117.64 walipoteza maisha, hatua iliyoifanya Tanzania kushika nafasi ya 87 duniani kati ya nchi takribani 200 zilizopimwa katika utafiti huo.

Nafasi ya JKCI kuokoa maisha Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani katika viwanja vya Taasisi ya JKCI jijini Dar es Salaam juzi, Dk Sanga alisema taasisi hiyo imekuwa inawaona zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku wakisumbuliwa na magonjwa ya moyo, wengi wao wakifika hapo wakiwa katika hatua mbaya ya ugonjwa. Siku ya Moyo Duniani huadhimishwa Septemba 29 ya kila mwaka.

“Ni magonjwa ambayo husababisha vifo vya watu wengi duniani huku hali ikionekana kuwa mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea.

“Tanzania hatujafanya utafiti wa kina lakini tangu taasisi hii imeanza kufanya kazi tunaona zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku na wengi huja wakiwa katika hatua mbaya ya ugonjwa, na tunawatibu,” alisema Dk Sanga.

Katika kile kinachodhihirisha ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo nchini, Dk Sanga anatoa mfano kuwa kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Moyo Dunia, taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Madaktari Afrika waliweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa 28 kuanzia Septemba 25 hadi Septemba 29, mwaka huu. 

“Tunawashauri wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kuweza kugundulika mapema iwapo wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya moyo au la,” alisema Dk Sanga.

Chanzo cha tatizo Akizungumzia chanzo cha magonjwa hayo ya moyo, mtaalamu wa lishe wa taasisi hiyo ya Jakaya Kikwete, Louiza Shem alisema mfumo mbovu wa maisha hasa ulaji usiofaa na kutokufanya mazoezi kunachangia watu wengi kupata magonjwa ya moyo. 

“Kwa bahati nzuri hakuna chakula ambacho mtu hatakiwi kutumia ili kujiepusha na magonjwa ya moyo, huwa tunashauri jinsi na kwa kiasi gani uvitumie ili kuepuka kupata magonjwa haya,” alisema. 

Akitoa mfano, mtaalamu huyo alisema; “Kuna vyakula vya wanga kama vile wali, ugali na vinginevyo, unakuta mtu anakula... amejaza sahani.

“Unapaswa kula kulingana na aina ya kazi unayofanya, kwa mfano wengi ambao tunafanya kazi ofisini hatutumii nguvu nyingi kulinganisha na wale wanaobeba mizigo, wengi tunakula nyama kwa kiwango kikubwa, ni vema kupunguza kiasi. 

“Mafuta yanayopatikana kwenye nyama yanaongeza uzito kupita kiasi na huenda kuziba mishipa ya damu, ikiwa ni ya kichwani utapooza mwili na ikiwa ni kwenye moyo utapata ‘heart attack’ (shambulio la moyo),” alibainisha. 

Alishauri pia jamii kupunguza kiwango cha chumvi kwani inapotumika kwa kiwango kikubwa huathiri afya ya moyo.

“Kundi kubwa tunaloona linaathirika na magonjwa haya ni wale waliopo kwenye umri wa uzalishaji na umri unavyozidi kuongezeka ndivyo uwezekano wa mtu kupata ugonjwa huu unavyoongezeka,” alisema. 

Dalili za ugonjwa Kwa mujibu wa wataalamu katika tasnia ya magonjwa ya moyo, ni kwamba mtu anaweza asione dalili za moja kwa moja za magonjwa ya moyo, hadi wakati mishipa ya damu ya moyo inapokuwa imeziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.

Inaelezwa kuwa mara nyingi, hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moja kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (heart attack/sudden death) au mtu anapopata kiharusi (stroke). 

Zaidi ya maelezo hayo ya wataalamu wa magonjwa ya moyo, dalili zinapojitokeza mapema hutofautiana kwa kutegemea aina ya ugonjwa wa moyo, ingawa dalili hizo nazo hazijitokezi mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine.

Hata hivyo, dalili kuu za magonjwa ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua upande wa kushoto (hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo); moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua; kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje. Dalili nyingine ni maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya; tumbo kujaa, kichefuchefu, na kutapika; kukosa usingizi; kupoteza fahamu.

No comments:

Post a Comment