WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (pichani) amesema
mauaji na uhalifu mkubwa, unaoendelea hapa nchini ni matokeo ya
kukosekana kwa misingi mizuri ya malezi kwa vijana, yenye kuzingatia
maadili ya dini na sasa amezitwisha ‘zigo’ asasi za kidini kusaidia
kudhibiti matukio hayo.
Mwigulu ambaye wizara yake ndiyo inayosimamia masuala ya ulinzi na
usalama wa raia na mali zao, alisema hayo juzi usiku kwenye Harambee ya
Kuchangia Fedha Kusaidia Ushirika wa Kiinjili wa Wanafunzi Wakristu Vyuo
Vikuu Tanzania (TAFES).
Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mwigulu aliweka wazi kuwa
matukio ya watu kuuawa, kutekwa, kuibiwa, kushambuliwa na kila aina ya
uhalifu unaoendelea nchini, chimbuko lake ni kukosekana kwa misingi
mizuri ya makuzi kwa vijana yenye hofu ya Mungu.
Alisema iwapo wazazi, walezi na viongozi wa dini, wakizingatia malezi
ya vijana katika misingi ya kidini, matukio hayo yatapungua kama sio
kuisha kabisa. "Serikali inatambua nafasi ya dini katika kuwalea vema
vijana watakaokuja kusaidia jamii na kuinua uchumi wa nchi, elimu ya
dini ndiyo njia pekee ya kukabiliana na uhalifu nchini," alisema.
Aliongeza; "Matukio ya uhalifu yanayoendelea nchini kwa sasa kwa
asilimia kubwa yanasababishwa na uwepo wa vijana wasio na malezi yenye
misingi ya kidini ambayo kimsingi ingewafanya kuwa na hofu ya Mungu na
kujikuta wakiepuka kutenda uhalifu, hivyo TAFES ni jukumu lenu kuwajenga
vijana tangu kwenye ngazi za vyuo."
Alisema, ili nchi isonge mbele ni lazima viongozi waandaliwe tangu
ngazi za vyuo vikuu, wanaposoma ili hatimaye waje kusaidia kusukuma
gurudumu la maendeleo ya nchi.
"Najua mtoto anajengewa misingi ya
kuongoza tangu akiwa shule ya msingi, pindi akijiunga na elimu ya chuo
hapati tabu kwa kuwa anakuwa tayari anajua kile anachotaka kuja kufanya
maishani, sasa hapo ndio muda muafaka wa kulelewa kwenye misingi ya
dini, hiyo itasaidia wingi wa wasomi wenye hofu ya Mungu watakaosaidia
taifa," alisema Mwigulu.
Pia Waziri Mwigulu alionesha kusikitishwa na watu ambao wanapinga
jitihada za Rais John Magufuli za kukabiliana na rushwa na kila aina ya
ufisadi nchini na kusema kuwa watu hao ni si adui tu kwa nchi, bali hata
kwa vizazi vijavyo.
Alisema viongozi waadilifu kama Rais Magufuli, si
tu muhimu kwa kizazi cha sasa, ila pia kwa vizazi vijavyo, hasa
ikizingatiwa kuwa anaandaa misingi ya taifa la vizazi vya sasa na
baadaye.
No comments:
Post a Comment