Sunday, October 1, 2017
Awamu ya pili ujenzi wa reli Standard Gauge kuanza Oktoba
Serikali imesaini mkataba na kampuni ya Yapi Merkezi kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya Reli ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR) kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kuanza Aprili, mwaka huu.
Hafla ya utiaji saini umefanyika leo (Ijumaa) katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) ikishihudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ikimuhusisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Yapi Merkezi, Erdem Arioglu.
Akizungumza kabla ya kusaini mikataba hiyo, Waziri Mbarawa amesema, reli hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kwani itachangia kushuka kwa gharama za bidhaa na hivyo kuleta unafuu wa maisha kwa watanzania.
“Watu wengi wanafikiri reli inajengwa siku moja, ujenzi wa reli unachukua muda mrefu na una hatua tano…serikali imedhamiria kuhakikisha reli ya kati inajengwa kwa kiwango cha Standard Gauge,” amesema Mbarawa.
Aidha, ameongeza kuwa serikali inaendelea kutafuta vyanzo vya fedha zaidi na mikopo nafuu isiyo na masharti magumu ili kuhakikisha mradi huo unajengwa. Jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya pili ya reli hiyo litawekwa mwishoni mwa mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment