Sunday, October 1, 2017

DC MWERA AFUNGA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA WILAYANI BUSEGA

Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi Tano Mwera leo tarehe Septemba 29, 2017 amefunga mafunzo ya Jeshi la Akiba wilayani humo kwa mwaka 2017.

Akiongea katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Wilaya alianza kwa kuwapongeza na kuwaasa vijana kuendelea kuwa watiifu, wakakamavu na wazalendo kama walivyofundishwa katika kipindi chote Cha mafunzo ikiwa ni Pamoja na kutii kiapo walichokula cha kuheshimu maamlaka zilizopo.

Mhe Mwera aliwasihii wahitimu kutotumia mafunzo hayo kwa kutenda maovu kama vile kujiunga na vikundi vya kihalifu vikiwemo vikundi vya ujambazi, wizi, kupiga watu mitaani n.k.

Aliwataka wahitimu hao kuwa mfano na kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yao.

"Mafunzo mliyopata yamewapa mwanga na kuwapa maarifa ya kujitegemea kimaisha hivyo basi tumieni maarifa mliyopewa katika kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali, msiende kuzurura mitaani". Alisema Mhe Mwera

Pia amewaomba wahitimu hao kusaidia kusimamia na kuelimisha jamii juu ya janga la wananchi kujichukulia sheria mikononi ikiwemo metendo ovu kama  vile kuua, na kutumiwa katika wizi. 

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Busega Mhe Tano Mwera Amewataka wananchi kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika na si kujichukulia sheria mikononi kwani kujichukulia sheria mkononi Ni Jambo la kihalifu na halipaswi kuungwa mkono.

Alitumia fursa hiyo pia kupiga marufuku Mtendaji yeyote au mwananchi kutoza faini watuhumiwa na kulipa vikundi vya watu wachache vinavyojiita wana mwano.

Alisema kuwa endapo itabainika mtu yeyote amechukua jukumu la kufungua mahakama yake anayoijua yeye hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mhe Mwera alisema kuwa Tanzania ni nchi ya Demokrasia na utawala wa sheria hivyo ina vyombo vyake vya dola vyenye uwezo wa kufanya kazi kubwa ya kuchunguza na kubaini matendo ovu kwa kushirikiana na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi.

No comments:

Post a Comment