Monday, September 11, 2017

WAZAZI WATAKIWA KUENDELEA KUWAKUZA WATOTO WAO KIMAADILI

JC9A0801
Wahitimu wa darasa la Saba katika shule ya Msingi Nalopa wakitumbuiza wageni mbalimbali wakati wa sherehe ya Mahafali iliyofanyika jana katika viwanja vya shule hiyo iliyopo jijini hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
JC9A0892
Wazazi na Walezi wa wanafunzi wa shule ya Msingi Nalopa wakimsikiliza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles Mkumbo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya Mahafali ya kuhitimu darasa la Saba (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
JC9A0983
Mgeni rasmi wa sherehe ya Mahafali ya darasa la Saba katika shule ya Msingi Nalopa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
JC9A1471
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akiwahutubia wageni waalikwa katika sherehe za Mahafali ya wanafunzi wa darasa la Saba wa shule ya Msingi Nalopa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
……………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Wito umetolewa kwa wazazi, na kuelezwa kwamba mbali na kujitahidi kuwasomesha watoto wao  katika shule mbalimbali kwa lengo la kuwapatia elimu bora wametakiwa pia kuzingatia kuwapa makuzi mema ili uhalisia wao kimuonekano uendane na elimu wanayoipata.

Hayo yameelezwa jana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Omari Mkumbo wakati wa sherehe ya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi Nalopa iliyopo jijini Arusha.

Kamanda Mkumbo ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo alisema kwamba, wanafunzi hao kwa sasa wanakwenda katika hatua nyingine ya kimasomo lakini pia umri wao unaongezeka na kukumbana na changamoto mbalimbali, hivyo wazazi wanatakiwa waendelee kuwakuza kimaadili ili elimu yao iwe na manufaa kwao na kwa jamii.

Alisema elimu wanayoipata ikiendana na maadili itawasaidia kuepuka kujiingiza katika vitendo vya uhalifu kama vile matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine wowote na hatimaye kuonekana kuwa wa thamani machoni mwa watu.

Kamanda Mkumbo aliwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika masomo yao hasa ya Sayansi ili idadi ya wataalamu wengi katika kada mbalimbali iongezeke hasa katika huu ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia ambao ushindani wa soko la ajira umekuwa mkubwa.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuwatunuku vyetu wahitimu hao ambao walifanya vizuri kimasomo, kinidhamu, uongozi, kimichezo na kujituma, Mlezi wa shule hiyo Balozi Mstaafu Bw. Daniel Ole Njoolay alitumia nafasi hiyo kumpongeza Kamanda huyo  kwa kuzidi kuimarisha hali ya usalama katika mkoa wa Arusha pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo.

Awali akizungumza katika Mahafali hayo Meneja wa shule hiyo yenye wanafunzi 461 Bw. Edward Njoolay alisema kwamba, awali akisoma wasifu wa shule hiyo alisema kwamba mwaka 1999 ilikuwa kama “Day Care” lakini ushawishi wa wazazi uliwawezesha kufanikiwa kufikia hatua kubwa kimiundo mbinu na kitaaluma.

Shule hiyo imefanikiwa kutoa wahitimu wa darasa la saba mara nane ukiondoa wahitimu wa jana na wote walifanikiwa kufaulu na kuendelea na masomo ya Sekondari ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya saba katika shule bora za Halmashauri ya jiji la Arusha zilizofanya mtihani wa darasa la saba.

No comments:

Post a Comment