Sunday, February 5, 2023

ISSA HAMIS ISSA MKAZI WA SHINYANGA APOTEA KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA TANGU NOVEMBA 2022


ISSA Hamis Issa (44), Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga ambaye anajishughulisha na ufundi wa magari amepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu novemba 2022 hadi sasa, Issa  anatafutwa na familia yake bila mafanikio.

Inadaiwa kuwa  mara ya mwisho aliondoka nyumbani kwao Mkoani humo bila ndugu kujua ameelekea wapi.

Hussein Hamiss ambaye ni mdogo wa Issa  alieleza namna ambavyo wamejitahidi kumtafuta ndugu yao bila kuwa na mafanikio yoyote mpaka sasa.

"Mwanzoni tulihisi kuwa kakaangu huenda akawa ameenda kwa ndugu na majamaa tukaanza taratibu za kuulizia na kufuatilia kwa ndugu wa karibu kwa muda wa zaidi ya wiki mbili lakini hatukupata majibu yoyote,"

"Hatukukata tamaa Tuliendelea kutafuta kwa watu wote wa karibu lakini hakukuwa na majibu yoyote ndipo tulipoamua kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha hapa Shinyanga nawao wakasema hawana taarifa zake ambapo tukapatiwa RB" SHY/RB/5459/2022,"

"Pia katika kuendelea kutafuta tulipata fununu kuwa ndugu yetu anashikiliwa na vyombo vya usalama kwaajili ya uchunguzi ila hatukujua ni uchunguzi wa nini na baadae tukaambiwa kuwa kesi yake iko hapa mkoa RCO anazo taarifa lakini kila tukitafuta ukweli kutoka kwa RCO hakuonesha ushirikiano,

"Polisi walisema kuwa watafatilia lakini kila tulipokuwa tukienda kufuatilia hakukuwa na majibu yoyote kuhusu ndugu yetu,tukafanya jitihada za kuonana na RCO lakini hakutupa ushirikiano wowote,"alisema Ndugu Hussen.

Alieleza kuwa mpaka sasa familia imekosa matumaini juu ya kupatarifa kutoka katika kituo cha polisi sababu ushirikiano sio mzuri akasema wanachotaka wao kufahamu nini kimemsibu ndugu yao waweze kufahamu kama yupo hai au laaa!

"Tumejaribu kufuatilia baadhi ya vituo vya polisi kama hapa Shinyanga,Mwanza pamoja na Dodoma lakini kote wanatupa majibu kuwa hayupo Wala hakuna taarifa yeyote inayomuhusu,"alisema Husseni.

Kwa upande wake Saida Issa ambaye pia ni mdogo wa ndugu Issa anaishi Dodoma alieleza kuwa alijaribu kufuatilia ndugu yake akiwa bila mafanikio.  

Anasema kuwa alienda kwa RPC wa mkoa wa Dodoma na kumueleza hali ilivyo lakini RPC alisema kuwa hawana taarifa wala hawajamshikilia mtu huyo.

"Mimi nikiwa Dodoma niliweza kufanikiwa kuonana na viongozi mbalimbali na kueleza ikiwa ni njia ya kuweza kusaidia kupatikana kwa kaka yangu lakini mpaka sasa bado ni kitendawili,

Mtu wa kwanza kumuwaza katika akili yangu ni RPC sababu tulisikia pia kuwa kunawatu walikamatwa shinyanga na wakaletwa Dodoma kwaajili ya uchunguzi lakini nilipofika kwa RPC aliniambia sio kweli hawana taarifa hizo,

Sikukata tamaa nilimtafuta Waziri wa mambo ya ndani lakini sikuweza kumpata ndipo nilipomtafuta Naibu wake na nikafanikiwa kuwasiliana naye akanambia atalifuatilia halafu atanipa majibu lakini majibu yake alisema kuwa kwa mkoa wa Shinyanga akiwasiliana na RPC na akamwambia ametafuta mahabusu zote zamkoa lakini hayupo,"alisema Saida.

No comments:

Post a Comment