Na Mathias Canal, Ushetu-Shinyanga
Serikali inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa mkopo wa
Shilingi milioni mia tatu sitini na moja na laki moja (361,100,000) kwa ajili
ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Ushetu
mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati akikabidhi
hundi katika hafla iliyofanyika Wilayani Ushetu tarehe 4 Februari 2023, Mbunge
wa Jimbo la Ushetu Mhe Dkt Emmanuel Peter Cherehani amesema kuwa fedha hizo ni
maelekezo ya serikali kwa Halmashauri zote nchini kutoa Asilimia 10 ya mapato
kwa ajili ya makundi hayo muhimu.
Dkt Cherehani amewataka
wanufaika hao wa mkopo kuhakikisha kuwa wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa
ili kujikwamua na wimbi la umasikini na si vinginevyo.
Amewasihi wanufaika hao
kutumia vizuri mikopo hiyo na kuhakikisha kuwa miradi waliyokusudia kutekeleza
wanaifanyia kazi ipasavyo ili waweze kurejesha mikopo kwa ajili ya kukopeshwa
watu wengine.
“Pelekeni fedha kwenye eneo
lililokusudiwa, ninajua wakati mwingine mnapata ushawishi kutoka kwa watu
wengine lakini fedha hizi sio za kwenda kuhonga, kafanyeni maendeleo yenu na
familia zenu” Amekaririwa Dkt Chereheni
Amesema kuwa fedha hizo
hazipaswi kuwa sehemu ya mtafaruku katika familia badala yake ziwe sehemu ya
kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya familia.
Pamoja na kukabidhi fedha
hizo kwa wanufaika hao pia Mhe Cherehani amekabidhi pikipiki kwa vijana kwa
ajili ya kufanya biashara ya Bodaboda itakayowaingizia kipato.
Amewasihi wanufaika hao
kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa
wakati.
Mikopo hiyo imetolewa kwa
vikundi 17 kati ya vikundi 70 vilivyoomba mikopo ambapo vikundi 11 ni vya
wanawake, vikundi vitano ni vya vijana huku kikundi kimoja kikiwa cha watu
wenye ulemavu.
Nao wanufaika wa mikopo hiyo
ambao ni wakazi wa Ushetu wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
mikopo hiyo kupitia Halmashauri za Wilaya huku wakisema kuwa watafanya kazi kwa
bidii ili kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
MWISHO
No comments:
Post a Comment