Monday, March 28, 2022

TAASISI YA AGA KHAN YAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI MWANZA KUHUSU UGONJWA WA SARATANI



Taasisi ya Aga khan nchini  kupitia mradi Mtambuka wa Saratani (TCCP) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)  imeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wahabari Mkoani Mwanza kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kuandika habari zinazohusu Saratani.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Jijini humo March 25, 2022 yakihusisha waandishi Zaidi ya 30 kutoka vyombo mbalimbali, Dkt Beda Likonda Daktari Bingwa wa Matibabu ya Saratani alisema kwa mwaka Tanzania inapata wagonjwa wapya 40,000 wa matatizo  ya saratani huku asilimia 10 ya wagonjwa hao ni saratani ya shingo ya kizazi, matiti, tezi dume na saratani nyinginezo. .

“ Kutokana na ukubwa wa tatizo hili tumeona sasa tuje kwa pamoja kuangalia namna ya kupambana na tatizo hili, hivyo tunawashukuru sana wenzetu wa taasisi ya Aga khan kupitia mradi wao wa TCCP kuona  kwamba iko haja ya kusimama pamoja kutoa elimu na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili” Alisema Dkt Beda

Alisema Changamoto ambazo wanazipata  katika hii tiba  maana yake wale wanaowaangalia wanaopambana na ugonjwa huo yaani  nchi za magahraibi kuna mihimili mikubwa minne ambayo wakiitendea haki wanaweza kupata matokeo mazuri.

Aliutaja Muhimili wa kwanza kuwa ni takwimu kwani takwimu za kwanza ni makisio, wa pili ni kinga ambapo  wanatakiwa kutoa elimu kuhusu kansa ni nini, chanzo chake,  inatokana na nini, tunajizuiaje nk na mhimili wa tatu ni tiba ambapo serikali inatakiwa kuhakikisha  kuanzia katika hatua mbalimbali za vituo vya tiba kama  zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa kuwepo na huduma  za kuwafikia  wananchi.

“ Na mhimili wanne ni tiba shufaa pale mgonjwa anaporudi nyumbani na hakuna uwezo wa kumtibu  basi  hata ikitokea amefariki, afariki awe hana matatizo mengi yaani ubora wa afya  yake ushughulikiwe .” Aliongeza  Dkt Beda

Alisema katika mihimili minne kuna mapungufu mengi wamefurahi watu wa Aga Khan wakishirikiana na wafaransa kuungana ili kuona wanaifikiaje hii mihimili yote minne na watakuwa wameanza na mihimili miwili wakiamini baadae wanaweza kuikamilisha mingine miwili ili waweze kupigana vizuri na adui Saratani(Kansa).

Akitoa mafunzo hayo kwa waandishi Dkt Athanas Ngambakubi Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka hospitali ya Mkoa Sekouture alisema katika Tanzania saratani ya Shingo ya kizazi kwa wanawake ndiyo inayoongoza ambapo kwa mwaka 2020 yaliripotiwa maambukizi mapya 10,241 ambayo ni sawa na asilimia 25.3 na vifo asilimia 24.2

Alizitaja dalili zake kuwa ni kutoka damu ukeni isivyo kawaida na tofauti na hedhi, kupata hedhi yenye damu nyingi na maumivu Zaidi ya kawaida na maumivu, kutoka damu ukeni wakati au baada ya kujamiiana na mwenza na pia kutoka majimaji ukeni isivyo kawaida na yenye harufu mbaya.

Dalili zingine ni maumivu ya kiuno, nyonga na mgongo pamoja kuchoka mara kwa mara.

Alisema uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi ni kumwangalia mama kwa kutumia kifaa kiitwacho speculum lakini kwa wenye umri Zaidi ya miaka 30 lakini kwa wenye umri chini ya huo hawazuiliwi kwenda kufanyiwa uchunguzi.

Aidha alisema Serikali imeendelea kuchukua tahadhari mbalimbali dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo chanjo iliyotolewa kwa mabinti kuanzia miaka 9 lakini pia namna ya kujikinga ikiwemo kuepuka ngono katika umri mdogo.

“ Licha ya kuwa saratani ni hatari tunaweza kuepuka maambukizi kwa kuepuka ngono katika umri mdogo, kuwa na mwenza mmoja mwaminifu, kutumia kondomu wakati wa kujamiiana, kula mbogamboga na matunda kwa wingi pamoja na kuacha matumizi ya tumbaku na kupunguza matumizi ya Pombe.” Alisema Dkt Athanas

Nao waandishi waliohudhuria mafunzo hayo waliishukuru sana taasisi ya Aga Khan kwa kuwapa mafunzo hayo kwani yatawaongezea ufahamu Zaidi katika kuandika habari zinazohusu ugonjwa wa saratani.

Mmoja wa waandishi hao Alphonce Tonny kutoka Yuhoma tv  alisema alikuwa akiifahamu Saratani  lakini hakujua kama kuna aina mbalimbali za Saratani  na matibabu yake.

“ Ukweli nilikuwa najua kuna Saratani  lakini nilikuwa sijui kama  kuna aina mbalimbali, uchunguzi wake, sababu zake na tiba zake kupitia mafunzo haya naamini uandishi wangu utabadilika sana na sasa jamii itafahamu kwa undani Zaidi na kwa kina kuhusu ugonjwa huu na mimi kama mwandishi ntatumia taaluma yangu kuondoa Imani potofu iliyojengeka kwa jamii na hata ofu juu ya ugonjwa huu kwamba ukiupata hauwezi kupona kumbe kuna watu wanaugua na kupona.” Alisema Alphonce   

Mradi Mtambuka wa Saratani wenye thamani ya Euro 13.3 unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD)  na Aga Khan Foundation(AKF) una lengo la kuboresha miundombinu na vifaa tiba vya huduma ya saratani, kuendeleza na kukuza rasilimali watu wa taaluma mbalimbali za matibabu ya saratani, kuboresha huduma na uhamasishaji wa saratani katika jamii na kudumisha ushirikiano na tafiti kuhusu saratani nchini.

Aidha utatekelezwa katika wilaya 13 za Mikoa ya Mwanza na Dar es salaam katika kipindi cha miaka minne ambapo kwa kushirikiana na timu za mikoa hiyo itaboresha huduma za awali za saratani katika vituo 100 ( 50 Dar es salaam / 50 Mwanza ) vya afya, huku manufaa yake yakitajwa kuenea nchi nzima.

Baadhi ya mafanikio hayo ni kufungwa kwa mashine ya kisasa ya Ultrasound katika taasisi ya Ocean Road yenye thamani ya Tzs 150 milioni ambayo inahudumia takribani wagonjwa 50-80 kwa siku, uwepo wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti(3D Mammography Machine) yenye thamani ya Tzs 800 milioni ambayo inahudumia wagonjwa takribani 20-25 kwa siku.

No comments:

Post a Comment