Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akisalimiana na Majaji wa Mahakama Kuu, Zahra Maruma na Ilvin Mgeta alipotembelea Kituo cha Huduma jumuishi kilichoko Temeke, mkoani Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu, akikagua ndani ya Jengo la huduma jumuishi litakalotumika kwa ajili ya msaada wa kisheria kwa mashauri ya ndoa, miradhi ta talaka na watoto lililoko Temeke mkoani Dar es Salaam, Kulia ni Mkuu wa Kituo hicho, Jaji wa Mahakama Kuu, Zahra Maruma na Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara, Lucy Saleko.
Mwonekano wa Jengo la Kituo cha Huduma Jumuishi litakalotumika kwa ajili ya usuluhishi na mahakama kwa masuala ya ndoa, mirathi, talaka na watoto lililoko Temeke mkoani Dar Es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Inaelezwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa iliyoghubikwa na mkinzano wa masuala ya kijamii ambapo tangu mwaka 2017 mashauri 7000 ya mirathi na mashauri 2000 ya migogoro ya ndoa yamefunguliwa.
Wananchi wa Mkoa wa huu walio katika migogoro ya Ndoa, mirathi na talaka wanakaribia kupata suluhu ya changamoto zao kwa wakati kufuatia kuanzishwa kwa Kituo jumuishi kwa ajili ya huduma hiyo.
Hayo yamebainika leo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu ya kukagua ukamilishaji wa kituo hicho, kilichopo Temeke mkoani Dar es salaam kinachotarajiwa kutoa huduma kwa wakazi wa Wilaya zote za mkoa huo.
Dkt. Jingu amesema kuwa hii ni hatua muhimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi hasa ukizingatia masuala ya mirathi na migogoro ya ndoa na familia imekuwa ikishamiri katika jamii.
“Serikali imeamua kuanzisha vituo jumuishi vya masuala ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa, mirathi na familia ili kuhakikisha mashauri haya yanapatiwa ufumbuzi kwa wakati” alisema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa kuanzia mwezi wa kumi mwaka huu wananchi wanaalikwa kupata huduma katika kituo hicho kwani mtu akishatoka katika kituo hicho atakuwa amepata jawabu la changamoto zake.
Dkt. Jingu amefafanua kwamba, vituo kama hivyo vitajengwa pia katika maeneo mengine nchini ili kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi katika masuala ya mirathi na kutatua migogoro ya ndoa.
Aidha Dkt Jingu amemshauri Mkuu wa Kituo hicho kuona uwezekano wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utatuzi wa mashauri ya ndoa, mirathi na talaka ili haki ipatikane kwa haraka na kuondokana na mlundikano wa mashauri .
Naye Mkuu wa Kituo hicho, Jaji Zahra Maruma amesema kituo hicho kitawezesha kuharakishwa kwa usuluhishi na kesi zinazohusu ndoa, mirathi na talaka hivyo kuokoa muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
“Kituo hiki kitatoa huduma ya mashauri ya mirathi ndoa na talaka na watoto na kitajumuisha wadau wanaotoa huduma zinazoendana na hizo” alisema
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Ilvin Mgeta amesema ziara ya Katibu Mkuu Dkt. Jingu Kituoni hapo ni hatua muhimu kutokana na dhamana anayoisimamia kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii hivyo itaongeza ushirikianao baina ya Wizara na Kituo hicho ili kusadiana katika kutatua changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa masuala yanayolengwa pia yanahusisha mustakabali wa watoto na pamoja na Ustawi wa Jamii kwa ujumla wake hivyo, Wizara yenye dhamana ina jukumu la kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora na kwa uharaka.
No comments:
Post a Comment