Friday, April 9, 2021

BUNGE LASITISHA ZIARA ZA MAFUNZO KWA WANAFUNZI NA MAKUNDI KUEPUKA MSONGAMANO

Bunge la Tanzania limesitisha ziara za mafunzo kwa wanafunzi na makundi mengine ili kuepukana na msongamano wakati wa Bunge la bajeti.

Aidha, limewataka wabunge kupeleka orodha ya wageni bungeni wasiozidi watano kwa kibali maalum cha ofisi ya Katibu wa Bunge.

Naibu Spika Dkt.Tulia Ackson ameyasema hayo bungeni wakati akisoma tangazo lililotolewa Katibu wa Bunge Stephen Kigaigai mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Amefafanua kuwa ofisi ya Katibu wa Bunge imeweka utaratibu huo kwa ajili ya kulinda afya za wabunge pamoja na watumishi katika kipindi hiki cha Bunge la bajeti ambapo wamekuwa wakipokea wageni wengi na hivyo msongamano kuwa mkubwa.

Amesema wameweka utaratibu huo kwa lengo la kudhibiti msongamano wa wageni bungeni kwa ajili ya kukabiliana na msongamano na kulinda afya za wabunge na watumishi wa Bunge.

“Kutokana na tangazo hili, wabunge wataruhusiwa kupeleka wageni wasiozidi watano bungeni kwa kibali maalum cha ofisi ya Katibu wa Bunge,”alieleza.

Naibu Spika amesema kuwa kila mbunge atatakiwa kupeleka maombi yake katika ofisi hiyo ambapo wataangalia ni wageni wangapi wapo kwa siku na kama watapata nafasi siku hiyo.

Aidha, amesema wizara itatakiwa kupeleka bungeni watendaji wasiozidi 15 ili kusaidia wakati wa Bunge la bajeti wakati bajeti husika wizara.

Baada ya kutoa tangazo hilo, amesisitiza kuwa ziara za mafunzo kwa wanafunzi na makundi mengine ya jamii zimefutwa na kuwataka wabunge kutoa ushirikiano.

MWISHO

No comments:

Post a Comment