Friday, April 9, 2021

WAZIRI UMMY AAGIZA WAWEKA HAZINA KATIKA HALMASHAURI ZILIZOPATA HATI MBAYA KUCHUKULIWA HATUA

Serikali imeziagiza Ofisi za wakuu wa mikoa na mamlaka za nidhamu kuwachukulia hatua waweka hazina waliohusika na uandaaji wa taaarifa za hesabu za mwisho katika halmashauri nane zilizopata hati mbaya na 53 zenye hati zenye mashaka.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe Ummy Mwalimu wakati akizngumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dodoma.

Ummy, ameagiza kuchukua hatua wakuu wa vitengo vya ukaguzi wa ndani wa halmashauri 54 ambao hawakukagua taarifa za hesabu za mwisho kabla ya kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ummy amesema kuwa hoja nyingi zilizotajwa na CAG zinatokana na baadhi ya watumishi wa halmashauri kutowajibika ipasavyo au kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.

Amesema kuwa waweka hazina hao waliohusika na uandaaji wa taarifa za hesabu za mwisho hawakutekeleza kikamilifu wajibu wao wa kutunza kumbukumbu za fedha na kuandaa taarifa sahihi jambo ambalo ni kinyume na memoranda ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009 Agizo la 27(3).

Kutokana na changamoto hizo alizitaka Halmashauri ziliopata hati mbaya na zeye shaka ziwabainishe wataalam wa fedha wenye CPA (T) ambao walisaini taarifa za hesabu za mwisho kuthibitisha kwamba taarifa hizo ni sahihi na hazina makosa.

Aidha, ameongeza kuwa wataalam hao wafikishwe bodi ya wahasibu na wakaguzi (NBAA) ili wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa taaluma zao.

Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanavijengea uwezo wa kuvitumia ipasavyo vitengo vya ukaguzi wa ndani kwa kuwapatia mafunzo ya mifumo ya kielektroniki, kuwatengea bajeti za kutosha na kutekeleza kwa wakati mapendekezo yote wanayotoa ili wakati wa ukaguzi kusiwe na dosari.

Kuhusu upotevu wa mapato, Waziri Ummy amezitaka ofisi za wakuu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha zinaimarisha usimamizi wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mapato yote yaliyopo mkononi yanapelekwa benki.

”Natoa siku tatu hadi jumanne mawakala wa wahakikishe wanawasilisha benki fedha zote walizonazo mikononi ili kuondokana na wizi wa mapato,”alisema Ummy.

Wakati huohuo, Ameagiza kupitiwa upya kwa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato ya halmashauri kwa lengo la kufanyia kazi dosari zote zilizobainishwa na CAG kuhusu mfumo huo.

Ameongeza kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa sasa vihusishe uwekaji mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa uendeshaji wake.

”Katika kuhakikisha kuwa ofisi a wakuu wa mikoa zinaongeza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kuzisimamia halmashauri, ninakusudia kuandaa na kusaini mikataba ya ufanisi kati yangu na wakuu wa mikoa wote nchini,”alisisitiza.

 MWISHO

No comments:

Post a Comment