Wednesday, March 31, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN APANGUA BARAZA LA MAWAZIRI

Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akitia saini Hati ya Kiapo mara baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kushuhudia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisoma majina ya Mawaziri na Manaibu Waziri aliowateua katika Baraza la Mawaziri mara baada ya kushuhudia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge Job Ndugai, mara baada ya hafla ya Uapisho iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

 

Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya Uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango wakiwa katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 31 Machi 2021. PICHA NA IKULU.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na Kutegua uteuzi wa Balozi Dk.Bashiru Ally na kumteua Katibu Mkuu Kiongozi Mpya.

Rais Mhe.Samia amefanya  mabadiliko hayo leo Machi 31,2021 Ikulu Chamwino Dodoma wakati wa hafla ndogo ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Katika uteuzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi wa Tanzania nchini Japan, Hussein Yahya Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Dk. Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge.

Kwa upande wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan amemhamisha aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu kwenda Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Selemani Jafo amepelekwa kushika nafasi ya Ummy Mwalimu.

Mwigulu Nchemba amepelekwa wizara ya Fedha na Mipango akisaidiwa na Hamad Masauni na nafasi yake katika Wizara ya Katiba na Sheria imechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Paramagamba Kabudi akisaidiwa na Jofrey Mizengo Pinda.

Amemteua Balozi Liberata Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa., huku Naibu wake akiteuliwa kuwa Mbarouk Nassoro Mbarouk.

Kwa upande wa Wizara ya Nchi ofisi ya Rais, utumishi na Utawala bora, ameteuliwa Mohamed Omary Mchengelwa,na Manaibu wake wakiwa ni Mwita Waitara pamoja na  Deogratius Ndejembi huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Capt. George Mkuchika atabaki Ofisi ya Rais atapangiwa kazi.

Wizara ya Uwekezaji imerejeshwa katika ofisi ya Waziri Mkuu na kutolewa ofisi ya Rais, huku Godrey Mwambe akiteuliwa kuwa Waziri wa wizara hiyo na Prof. Kitila Mkumbo akipelekwa wizara ya Viwanda na Biashara na Naibu wake akibaki yule yule Mhe. Exaud Kigahe .

Pia amemhamishia Pauline Gekul  kuwa Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, huku aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega akipelekwa wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa naibu waziri.
Pia amehamishia Mwanaidi Ally Hamis  kuwa naibu waziri wa pili katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
 
Akitangaza mabadiliko hayo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuondoka kwa Dk. Philip Mpango katika Wizara ya Fedha na Mipango kumempa nafasi ya kulitazama baraza lote la mawaziri na kufanya mabadiliko kidogo.

Nimeona niwabadilishe kwa sababu tangu mumeapa ni muda mfupi kuona nani ameshindwa, tunaanza na hawa awamu ya sita, jinsi tunavyokwenda tutaona nani tunakwenda nae na nani tunamuacha.

Naibu mawaziri mkatumike vizuri, kuna kudharauliana, naibu anadharau waziri na waziri nae anadharau naibu, kazi ni kazi sitaki kusikia kingine,” amesisitiza.

Katika upande mwingine, Rais Samia amefanya uteuzi wa wabunge watatu ambao ni Dk. Bashiru Ally, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk.

Akimuelezea Dk.Philip Mpango ,Rais Mhe. Samia Suluhu  amesema kuwa Dk. Mpango ni mcha Mungu, mchumi mahiri, mchapakazi, mzoefu, hodari na hana Mambo mengi.

Ameeleza  namna alivyomuamini Dk. Mpango na kuamua kuteua jina lake, Huku akikishukuru chama chake kwa kumuunga mkono na kulipitisha jina hilo.

“Nilizunguka sana kupata jina, nikaangalia ndani na nje ya Bunge, na mtu niliyemuona anafaa ni ndugu yetu Philip Mpango,Philip nilimkuta ametulia nikaona ndiye anafaa,majina mengine nilikuta yana hili mara lile,naamini atanisaidia kwenye uchumi na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali,”amesisitiza.

Rais Samia amesema kuwa zenge hailali kesho majira ya saa nne asubuhi Mawaziri na Manaibu wataapishwa Ikulu Chamwino Dodoma.

No comments:

Post a Comment