Tuesday, March 30, 2021

USIYOYAJUA KUHUSU KIWANJA CHA NDEGE SONGEA



LICHA ya kwamba mengi yameandikwa kuhusu kiwanja cha ndege cha Songea kilichopo Ruhuwiko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,bado kuna mengi yanayokihusu kiwanja hiki.

Historia inaonesha kuwa kiwanja cha ndege cha Songea kilianzishwa mwaka 1950 ambacho kilikuwa kinamilikiwa na mtu binafsi aliyefahamika kwa jina moja la Robert.

Meneja wa Kiwanda cha Ndege Songea Jordan Mchami anasema ilipofika mwaka 1963 serikali ilichukua umiliki wa ,kiwanja hicho kutoka kwa mtu binafsi na kuanza kukiendesha kiwanja hicho.

Hata hivyo anasema wakati serikali inakichukua kiwanja hicho,barabara ya ndege ilikuwa ni ya vumbi na kwamba ilipofika mwaka 1979,serikali iliona umuhimu wa kukikarabati kiwanja hicho kwa kukiwekea lami.

“Wakati serikali inakarabati kiwanja hicho kwa kukiwekea lami ,barabara ya ndege ilikuwa na urefu wa meta 1625 na upana wa meta 30,uwanja uliendelea kutumika kwa kutumia ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria 13’’,anasema Mchami.

Kwa mujibu wa Meneja huyo,ilipofika mwaka 2017,barabara ya ndege katika kiwanja cha Songea ilikuwa imechakaa sana hivyo serikali iliona umuhimu wa kukarabati kiwanja hicho kwa kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege toka urefu wa awali wa meta 1625 kwa upana wa meta 30 na kufikia meta 1740 ambapo upana wake ulibakia meta 30.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lasack Alinanuswe anasema ukarabati wa kiwanja hicho. umetekelezwa na kampuni ya CHICCO kutoka nchi ya Jamhuri ya China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara TANROADS kwa gharama ya shilingi bilioni 37.

Anazitaja kazi ambazo zimehusika kwenye ukarabati  na upanuzi wa kiwanja hicho kuwa ni urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka ndege kutoka meta 1625 hadi meta  1740.

Hata hivyo anabainisha kuwa  mwisho wa pande zote za kutua ndege kuna eneo la usalama(Stop way) lenye urefu wa meta 60 kila upande hivyo kufanya barabara yote kuwa na urefu wa meta 1860

Kulingana na Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni   eneo la maegesho madogo ya ndege yenye ukubwa wa meta 70 kwa meta 40 na kwamba matumizi ya maegesho hiyo ndogo ya ndege ni kuegesha ndege za dharura na ndege za kijeshi.

Mhandisi Alinanuswe anasema katika kiwanja hicho kumejengwa maegesho kubwa ya ndege yenye uwezo wa kuegesha ndege sita kubwa aina ya bombardier kwa wakati mmoja yenye urefu wa meta 139 na upana wa meta 126.

Hata hivyo anasema maegesho ya ndege ya zamani  ilikuwa ni ndogo yenye urefu wa meta 72 kwa meta 55 na kwamba katika ukarabati huo,limejengwa jengo jipya kwa ajili ya abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria kati ya 150 hadi 200 ambapo jengo la zamani la abiria lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi abiria 75 tu.

Meneja Kiwanja cha Ndege Songea,anazitaja fursa zilizopo katika kiwanja hicho kuwa ni  maeneo ya kupangisha wawekezaji kwa ajili ya kuweka maduka,hoteli pia kuna maeneo ambayo kiwanja cha ndege Songea kinaweza kuingia ubia kwa kutoa ardhi na wawekezaji kujenga na baada ya kumaliza mkataba eneo linabaki kuwa mali ya kiwanja cha ndege.

Anaitaja fursa nyingine inayopatikana kwenye kiwanja hicho,ni fursa ya biashara ya taksi kwa ajili ya kusafirisha abiria toka katika kiwanja cha ndege hadi mjini Songea.

Akizungumzia mwenendo wa abiria tangu kurejeshwa kwa safari za abiria za ndege za ATCL Feburiari 17 mwaka huu,Meneja Kiwanja cha Ndege Songea anasema mwitikio wa abiria ni mzuri kwa sababu ndege iliyokuwa inatoa huduma kabla ya ATCL ilikuwa ni ndogo yenye uwezo wa kubeba abiria 13 tu na nauli yake kwenda pekee ilikuwa ni zaidi ya shilingi 500,000.

“Hivi sasa kupitia ndege ya serikali za ATCL yenye uwezo wa kubeba abiria 76,nauli kwenda tu ni shilingi 250,00,kwenda na kurudi ni shilingi 370,000 kwa hiyo abiria wamepunguziwa mzigo wa nauli’’,anasema Mchami.

Anasisitiza kuwa kutokana na hali hiyo siku hadi siku idadi ya abiria inaendelea kuongezeka ambapo hivi sasa ratiba ya ndege ni mara mbili kwa wiki,siku za Jumatano na Jumapili ambapo uzoefu unaonesha kuwa siku ya Jumapili kunakuwa na idadi kubwa ya abiria.

“Tunatarajia kuwasiliana na ATCL Makao makuu kuona uwezekano  wa kubadilisha ratiba ya ndege ikiwezekana iwe siku za Jumatatu,Jumatano na Ijumaa ili Ijumaa jioni  watu wanaweza kutoka kazini kuamua kusafiri na Jumatatu Asubuhi kurejea kazini Songea, kwa kifupi idadi ya abiria inaridhisha’’,anasisitiza Mchami.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme anasema kiwanja cha ndege  wa Songea ni rasilimali adimu inayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea na Mkoa mzima wa Ruvuma hasa kukuza sekta ya utalii,baada ya kuanzishwa mpango mkakati wa kukuza utalii katika mkoa wa Ruvuma.

No comments:

Post a Comment