Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba (kushoto), akimkaribisha Katibu Mteule wa Tume hiyo, Mwl. Paulina Nkwama katika Ofisi yake mpya, Makao Makuu ya Tume, Dodoma, baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (kulia), akimkabidhi Katibu Mteule wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama, Ripoti kuhusu Tume husika, wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Ofisini kwake, Makao Makuu Dodoma, baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.
Katibu Mteule wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama, akiendelea na majukumu Ofisini kwake, Makao Makuu Dodoma, muda mfupi baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.
Katibu Mteule wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama (aliyesimama), akizungumza na Wajumbe wa Menejimenti, Makao Makuu Dodoma, muda mfupi baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa TSC, Prof Willy Komba na kushoto kwake ni aliyekuwa Kaimu Katibu, Moses Chitama.
Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wakimpokea Katibu Mteule wa Tume hiyo, Mwl. Paulina Nkwama, alipowasili kuanza kazi rasmi, Aprili 1, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape (kushoto), akiwasilisha salamu za ukaribisho kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote, kwa Katibu Mteule wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama (kulia), baada ya kuripoti rasmi Makao Makuu Dodoma na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Shani Kamala, akiwasilisha Taarifa kuhusu Tume kwa Katibu Mteule wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama (hayupo pichani), alipokutana na Menejimenti baada ya kuripoti rasmi Makao Makuu Dodoma na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.
Katibu Mteule wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama (kushoto), akimshukuru kwa kumfikisha salama na kuagana na aliyekuwa Dereva wake, Sajenti Martin Mwanandota, baada ya kuripoti rasmi Ofisi yake mpya, Makao Makuu Dodoma, Aprili 1, 2021. Kabla ya uteuzi wake, Mwl. Nkwama alikuwa Katibu Tawala Msaidizi (Elimu), Mkoa wa Kilimanjaro.
Veronica Simba na Adili Mhina
Katibu Mteule wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwalimu Paulina Nkwama, leo Aprili 1, 2021 ameripoti Ofisini kwake, Makao Makuu ya Tume, jijini Dodoma na kuanza kazi rasmi.
Mwl. Nkwama ameanza majukumu yake baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo kuanzia Machi 29 mwaka huu, akichukua nafasi ya Winfrida Rutaindurwa ambaye amemaliza muda wake.
Akizungumza na Menejimenti ya TSC, muda mfupi baada ya kuwasili ofisini hapo, Mwl. Nkwama amesisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi ili kwa pamoja waweze kutimiza azma ya kuihudumia vyema kada wanayoisimamia, yaani Walimu walio katika Utumishi wa Umma.
“Kwenye Taasisi kukiwa hakuna upendo ni changamoto, hivyo nawaomba tupendane, tushirikiane na tushikamane. Tukienda hivyo, naamini kwa msaada wa Mungu, tutafanikiwa.”
Aidha, Katibu Mteule Nkwama ametumia nafasi hiyo kueleza shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha katika hatua mbalimbali za maisha yake hadi kufikia mahali alipo na pia amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumwamini na kumteua kushika wadhifa husika.
“Naamini Mheshimiwa Rais aliwaona wengi ambao wana sifa za kushika wadhifa huu, lakini akaniamini mimi na kunipa nafasi ya kuwatumikia Watanzania hususani Walimu ambao Tume hii inawasimamia. Namshukuru sana na ninaahidi sitamwangusha,” ameeleza Mwl. Nkwama.
Vilevile, amewataka watumishi wote wa TSC kutambua kuwa yeyé ni mtumishi mwenzao hivyo waachane na kasumba za kumwogopa kutokana na wadhifa wake. Badala yake amewataka wawe huru kushirikiana naye katika kazi huku akiahidi kupokea ushauri kutoka kwa yeyote na kuufanyia kazi ili kupata matokeo chanya.
Kwa upande wake, akimkaribisha Katibu Mteule, Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba amempongeza kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo.
Aidha, Prof. Komba amemweleza Katibu Mteule Nkwama kuwa Menejimenti ya TSC ina Wajumbe mahiri wenye weledi na utendaji mahiri wa kazi, hivyo anaamini kupitia uongozi wake, Tume itaendelea kufanya kazi nzuri.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi ya ukaribisho, aliyekuwa Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama ameeleza kuwa Tume imepokea uteuzi wa Mwl. Nkwama kwa furaha kubwa na kwamba wana imani naye.
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote, Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu Christina Hape, ameahidi kuwa watampatia ushirikiano Katibu Mteule ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Awali, akiwasilisha Taarifa fupi kuhusu TSC kwa Katibu Mteule, Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Shani Kamala, alibainisha jukumu kuu la Tume kuwa ni kuendeleza na kusimamia Utumishi wa Walimu.
Kabla ya uteuzi wake, Mwl. Nkwama alikuwa Katibu Tawala Msaidizi (Elimu), Mkoa wa Kilimanjaro. Zoezi la kuapishwa kwake linatarajiwa kufanyika siku yoyote kutoka hivi sasa baada ya taratibu husika kukamilika.
No comments:
Post a Comment