Sunday, December 6, 2020

WANANCHI WATAKIWA KUILINDA MIUNDOMBINU YA MAJI

Wananchi wa Jimbo la Ilemela wametakiwa kulinda miundombinu ya maji inayoendelea kujengwa na kukarabatiwa jimboni humo ili kuondokana na adha ya kukosekana kwa huduma ya upatikanaji wa maji.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa ndani ya Jimbo lake ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa tenki la maji lililopo kata ya Kahama-Buswelu jirani na mlima wa kwa mkuu wa wilaya na Ujenzi wa Stendi ya kisasa ya mabasi na malori kata ya Nyamhongolo ambapo amewaasa wananchi waliojirani na mradi huo wa maji kuhakikisha wanalinda na kutunza mradi huo  mkubwa wa tenki la maji sanjari na kutolea taarifa kwenye mamlaka husika za Serikali vitendo vyote vya kiuharifu na uhujumu vitakavyotekelezwa na watu wasiokuwa na nia njema

'.. Serikali imewekeza pesa nyingi ili mwananchi wake aondokane na adha ya ukosefu wa maji na apate maendeleo alafu mwananchi mwenyewe anaenufaika anaenda kuiba vifaa  kama saruji na vyenginevyo vinavyotumika kujengea, Huko ni kukwamisha maendeleo yako mwenyewe niwaombe wenyeviti wa mitaa na wananchi wote kusimamia hili ..' Alisema

Aidha Dkt Mabula akaelekeza kuwa vibarua wa kazi zisizohitaji utaalamu sana wachukuliwe kutoka miongoni mwa wananchi wanaoishi jirani na mradi huo ili iwe rahisi kwa wananchi hao kuthamini na kulinda mradi huo mbali na kujikwamua kiuchumi kutokana na fedha watakazolipwa katika kufanya kazi hapo.

Kwa upande wake  msimamizi wa mradi huo Mhandisi Gogadi Mgwatu akasema kuwa mitaa itakayonufaika na mradi huo ni Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba, Kahama, Bujingwa, Nyamadoke na Ilalila sambamba na kuongeza kuwa mradi huo wa ujenzi wa tanki la maji unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Juni, 2021 ukitekelezwa na mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni Tano

Nae katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akafafanua kuwa Chama chake kina wajibu wa kuisimamia Serikali yake baada ya uchaguzi kutatua kero na changamoto za wananchi, Hivyo  kilichofanywa na Mbunge wa Ilemela Dkt Angeline Mabula kwa kushirikiana na Serikali ni kutekeleza kile kilichoahidiwa na Chama chake kwa wananchi baada ya kukiamini kupitia uchaguzi mkuu ilioisha hivi karibuni na kukipigia Kura nyingi. 

Akihitimisha Bi Jackline Masanja moja ya wananchi wa kata ya Kahama akampongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela na kuishukuru Serikali ya Rais Dkt John Magufuli kwa kuamua kutatua kero ya muda mrefu iliokuwa ikiwakabili ya ukosefu wa huduma ya maji.

No comments:

Post a Comment