Monday, December 7, 2020

KATIBU MKUU KUSAYA AFUNGA MAFUNZO YA KILIMO KWA VIJANA WA MKOA WA PWANI NA KUWAHAMASISHA KUJIAJIRI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiangalia bamia zilizopandwa na Vijana wanaopata mafunzo katika kambi ya Mkongo leo tarehe 7 Dsemba, 2020 wakati alipotembelea kambi hiyo pamoja na kufunga mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa Vijana 48 wanaotoka aktika Halmashauri za wilaya ya Mkuranga, Kisarawe, Kibiti, Rufiji na Bagamoyo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiwahutubia Vijana 48 walioshiriki mafunzo hayo kabla ya kufunga kambi ya mafunzo na kugawa vyeti kwa Wahitimu wake

Sehemu ya Vijana 48 kutoka Halmashauri tano za mkoa wa Pwani wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya hayupo pichani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akimkabidhi cheti mhitimu Bi. Saumu Issa kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga baada ya kufungwa kwa kambi hiyo ya mafunzo


Katibu Mkuu; Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya Leo mchana Tarehe 7 Desemba, 2020 amefunga mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa vitendo kwa Vijanza 48 wa mkoa wa Pwani; Hususan wanaotoka katika wilaya ya Bagamoyo, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji. Mafuzo yaliyoendeshwa kuanzia Mwezi Julai hadi Desemba, 2020 kupitia Ushirika wa waliowahi kusoma Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO).

Katibu Mkuu Kusaya amewahamasisha Vijana waliopata mafunzo ya kilimo na ufugaji wa kuku wa nyama na mayai kufikiria kujiajiri kwa kuanzia na mitaji midogo kwa kuwa juhudi zozote uanza kwa hatua ndogo na baadae safari ya ujasiliamali inakamilika.

“Kwa hali ilivyo; Serikali haina uwezo wa kuajiri Vijana wote nchini; Hiki tulichokifanya leo ni sehemu ya kuwatengenezea mazingira ili yawe rafiki kwa ninyi kujiajiri. Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipotamka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano; Itatengeneza ajira milioni nane (8) ni pamoja na ninyi kujiajiri kupitia Sekta ya Kilimo na Mifugo.”

“Tafuteni mikopo kwa ajili ya kuanzisha Miradi mbalimbali kupitia Halmashauri zenu kupitia mikopo ya Vijana (Asilimia 5) kina Mama (Asilimia 5) na Walemavu (Asilimia 2).”

“Undeni Vikundi na nendeni kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zenu; Mtapata mikopo na kama mtakutana na changamoto; Tutafuteni Sisi (Viongozi wenu nikiwepo Mimi Katibu Mkuu Kilimo).” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Akijibu changamoto zilizopo katika Kituo cha kilimo cha kambi ya Vijana ya Mkongo; Katibu Mkuu Kusaya ameagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Wizara ya Kilimo kufika katika Kituo cha Mkongo ili kufanya tathmini ya kuboresha mfumo wa maji kutoka Mto Rufiji.

Katibu Mkuu pia amemueleza Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO kuleta maombi rasmi  ya kuboreshewa bwalo la chakula, mabweni ya Vijana wanaolala Kituoni wakati wa kupata mafunzo.

Aidha; Katibu Kusaya ameahidi muda mfupi kuanzia leo kukipa Kituo cha Mkongo trekta dogo (Power Tiller) jipya, pikipiki mbili mpya pamoja na kutoa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa banda bora la kufuga kuku pamoja na kununua kifaa cha kutotolesha vifaranga (Incubator) kubwa na kusisitiza maombi ya uhitaji wa vifaa hivyo ufike ofisini Dodoma kwa maandishi haraka iwezekanavyo.

Mafunzo hayo yameendeshwa katika kambi ya Vijana iliyopo katika kijiji cha Mkongo, kata ya Mkongo wilayani Rufiji ambapo sehemu ya mafunzo hayo ilikuwa ya vitendo kwa asilimia 80 na nadharia kwa asilimia 20.

Katika taarifa yake kwa Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO Bwana Revocatus Kimario amesema; Wahitimu wamepata nafasi ya kujifunza namna bora ya kulima mazao ya bustani (Mbogamboga na Matunda), mafunzo ya kufuga kuku wa nyama na mayai, mafunzo ya utengezaji wa vyakula vya mifugo (Kuku wa nyama na mayai).

Naye Muhitimu wa mafunzo hayo kutoka wilaya ya Mkuranga Bi. Wisdom Samson ametoa ombi kwa niaba ya Wahitimu wenzake 48 kwa kumuomba Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya kupewa ardhi kutoka kwenye Halmashauri zao pamoja na kupewa mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara za kufuga kuku wa nyama na mayai lakini mwisho Wahitimu wameomba kudhaminiwa ili kupata mikopo ya bei nafuu kutoka kwenye Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO Bwana Revocatus Kimario amemweleza Mgeni Rasmi kuwa Taasisi yao imekuwa ikitumia Kituo cha Mafunzo Mkongo kuanzia mwaka 2015 na kwamba kuanzia muda huo hadi leo; SUGECO Imetoa mafunzo kwa Vijana zaidi ya 1,461 ambapo mafunzo hayo yanalenga kutoa mafunzo katika kilimo cha mazao ya bustani (Mbogamboga, matunda, maua na viungo) ufugaji wa kuku, ufugaji wa mbuzi, ufugaji wa nyuki pamoja na kilimo cha mazao ya mizizi.

SUGECO kwa kushirikiana na Wadau wengine imefunga miundombinu na teknolojia mbalimbali za kilimo ili kuwezesha utoaji wa mafunzo kwa vitendo hii ni pamoja na kufunga vitalu nyumba 7 (Greenhouses), kukarabati majengo ya Kituo, kuanzisha mashamba ya mfano (Demo farms) kwa kutumia mfumo wa kisasa wa umwagiliaji (Drip Irrigation systems) na mabanda ya kuku yenye uwezo wa kuweka kuku zaidi ya 1,000.

MWISHO

No comments:

Post a Comment