Monday, March 2, 2020

WAZIRI MWAKYEMBE AAGIZA MAADILI YA KITANZANIA YASIMAMIWE IPASAVYO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na washiriki wa Bonanza la kuibua vipaji vya uimbaji lililofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro lililoongozwa na kaulimbiu “Tutambue vipaji vyetu tujiajiri kufikia uchumi wa kati na JPM.”

Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule akitoa taarifa fupi juu ya tamasha la kuibua vipavi vya uimbaji wilayani humo kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuongea na hadhira iliyohudhuria bonanza hilo kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa sanaa kwa vijana na ajira ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kushoto) akimkabidhi maiki mwanafunzi Jamila Jafari (wa kwanza kulia) aliyefanikiwa kuimba wimbo wa mwanamuziki Elias Barnabas (Barnaba Boy, wa katikati) wa “Namtaka wife material ninayefanana naye”wakati wa Bonanza la kuibua vipaji vya uimbaji wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu pamoja na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wafanye kazi yao ya kisheria ya kulinda maadili ya jamii ya itanzania ili taifa liendelee kufuata misingi imarya utamaduni na sanaa iliyoasisiwa na viongozi wetu.

Dkt. Mwakyembe ametoa agizo hilo wakati wa mashindano ya Bonanza ya kuibua vipaji vya uimbaji lililofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro ambalo liliongozwa na kaulimbiu “Tutambue vipaji vyetu tujiajiri kufikia uchumi wa kati na JPM.”

Akizunumzia umhimu wa sanaa na utamaduni katika jamii Waziri amesema “Huwezi kuruhusu upuuzi huu unaendele wa kuharibu watoto wetu kabla hawajakua, haiwezekani kuanza kurusha vipindi vya ajabu ajabu asubuhi, tuna sheria tumepitisha Bungeni ipo wazi. Nyimbo zote zenye mashaka mashaka ambazo inabidi waangalie watu wazima zianze kupigwa kuanzia saa 6:00 usiku, ipo kwenye sheria situngi mimi sasa hivi na mwisho ni saa 11:00 alfajiri, tusijiachie hivi Watanzania, haiwezekani” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.

Waziri huyo mwenye dhamana ya sekta ya habari, amevitaka vyombo vya habari kwa washirikiane na BASATA, Bodi ya Filamu pamoja na Kamati ya Maudhui ya TCRA kutekeleza agizo hilo kwa kuzingatia ukweli kuwa kuna taifa ambalo lina wajibu wa kutekeleza na kuendeleza maadili ya nchi na hatua itakayosaidia kuwaendeleza na kutokuharibu watoto wadogo kwa kutekeleleza wajibu wa taasisi hizo wa kisheria.

“Naviagiza vyombo hiyo, hebu fanyeni kazi yenu, jamani tuwape watoto haki yao ili wakue kama sisi tulivyokuwa, haiwezekani mtoto mdogo wa miaka mitatu amekomaa ukimwangalia machoni amekomaa kwa ajili ya kuonyeshwa vitu vya ajabu ajabu vya kijinga. Nalisema hili sio kwa mzaha, kuanzia Machi 1, 2020 nikiona vyombo vyetu vya televisheni na redio maudhui yao yanakiuka maadili yetu halafu vyombo vyetu vinavyosimamia maadili vimekaa kimya, heri tuwabadilishe tuweke watu wapya waweze kufanya kazi ya kulinda maadili ya mtanzania” alisema Dkt. Mwakyembe

Aidha, Waziri amesisitiza kufurahishwa na washiriki wa Bonanza hilo la kuibua vipaji Same ambapo vikundi na washiriki wote wameonesha wananidhamu kwa kuzingatia maadili ya mtanzania ambayo wameyalinda, yanaendelezwa na kuwafanya waimbe vizuri wakiwa wamevaa mavazi ya heshima kulingana na maadili ya kitanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule amesema washindi wa bonanza hilo watapata fursa ya kurekodi kazi zao ambazo zitatumika katika vyombo vya habari ndani na nje ya nchi ambazo zitasaidia kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii.

Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira ya dhati aliyoionyesha katika kuinua wasanii kwa kutoa Shilingi milioni 100 mwaka 2019 kwa ajili ya kusaidia kazi za sanaa na amekuwa mfano wa kuigwa kila eneo ambapo na wao kama wasaidizi wa Rais wanaunga mkono katika maeneo yao ikiwemo Bonanza la kuibua vipaji wilayani Same.

Aidha, amesema kuwa Dkt. Mwakyembe amekuwa msatari wa mbele katika kutatua changamoto za wasanii ikiwemo maboresho ya Sheria zinazopelekea kulinda haki wasanii hatua inayowatia wasanii moyo kwa kutambua juhudi za Serikali katika kazi zao za sanaa. 

Naye Balozi wa Utalii na Mdau wa Maendeleo Tanzania Nangasu Werema amesema anaipenda nchi yake Tanzania na maendeleo yanayoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano na kuwahamasisha watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambapo kuna mradi endelevu wa kuhakikisha wanayama aina faru unaendelezwa na hatimaye kuchangia pato la taifa na hivyo kukuza uchumi wa nchi ambao unatajiwa kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo 2025.

Bonanza la kuibua vipaji vya uimbaji wilayani Same mwaka huu linafanyika kwa mara ya pili tangu kuanza kufanyika mwaka 2019 ambapo limekuwa na mafaniko mengi ikiwemo mwitikio wa wananchi wengi kushiriki bonanza hilo katika fani za nyimbo mbalimbali ikiwemo kwaya, bongo fleva, ushairi pamoja na ngoma za asili ambazo zilitafsiriwa katika maudhui ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, Mafannikio ya Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Utunzaji wa mazingira na kuendeleza utalii nchini.

No comments:

Post a Comment