Monday, March 2, 2020

WAZIRI MKUU AFUNGUA HUDUMA YA KUCHUJA DAMU


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Christopher Nyange mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika  kitengo cha kuchuja damu baada ya kufungua kitengo hicho katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mganga ya Bombo, Machi  1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipofungua kitengo cha kuchuja damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, Machi 1, 2020. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela,  wa tatu kulia ni Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wa pili kulia ni Mganga Mfawidhi  wa hospitali hiyo, Dkt. Naima Yusuf. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua kitengo cha kuchuja damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa  wa Tanga ya Bombo, Machi 1, 2020.  Wa tatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Mwita Waitara na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mradi wa huduma ya kuchuja damu  katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo na kupunguza gharama ya kuwasafirisha wagonjwa wenye matatizo ya figo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  kufuata hiduma hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amefungua mradi wa ujenzi wa barabara ya Makorora-Msambweni (km nne) iliyojengwa kwa thamani ya sh. bilioni 5.9 ambayo itarahisisha mawasiliano kwa wakazi wa kata za Msambweni, Makorora, Mzingani na watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Waziri Mkuu amezindua miradi hiyo kwa nyakati tofauti jana (Jumapili, Machi 1, 2020) wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara  ya kikazi mkoani Tanga, ambapo alisisitiza azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi wote. 

Alisema sekta ya afya imepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka minne iliyopita na Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na maboresho ya stahili za watumishi. Amewataka watumishi waendelee kuwa watulivu wawe na Imani na Serikali yao.

Alisema ni vema kwa watumishi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanafanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili wagonjwa wenye matatizo ya figo pamoja na matatizo mengine ya kiafya wapate huduma bora  bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao kuandaa utaratibu wa kutoa elimu kila siku asubuhi juu ya umuhimu wa kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na  yasiyoambukiza ambayo ni hatari na ya gharama kubwa.

“Suala la mazoezi ni tiba muhimu na nyie wataalamu ambao mnajua ugonjwa huu tunautibu vipi ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, hivyo  andaeni nafasi ya dakika tano hadi kumi za kutoa elimu na kuhamasisha watu wajenge tabia ya kufanya mazoezi. Magonjwa mengine yanaweza kutibika kwa kufanya mazoezi na kubadilisha mitindo ya maisha.”

Waziri Mkuu alisema Serikali imeboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi wake zikiwemo za afya, hivyo aliwaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali wahakikishe hakuna mwananchi anayekwenda kwenye maeneo ya kutolea huduma na kukosa dawa au vipimo.

Akizungumza kuhusu barabara ya Makorora-Msambweni, Waziri Mkuu alisema mbali na kurahisisha mawasiliano pia itaboresha usalama na mazingira ya wananchi kutokana na uwepo wa taa za barabarani jambo litakaloongeza thamani ya makazi.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema huduma za figo nchini zilikuwa zinatolewa katika vituo 19 vya binafsi na hospitali tano za Serikali ambazo ni Hospitali za Kanda za Rufaa Muhimbili, Mbeya, Bugando, KCMC na Benjamin Makapa.

Waziri Ummy alisema hadi 2016 asilimia 90 ya huduma za kusafisha figo zilikuwa zinatolewa na sekta binafsi na asilimia 10 taasisi za umma. “Hali hii inasababisha huduma za usafishaji figo kuwa na gharama kubwa na kukosa uwiano wa huduma hasa kwa wananchi waishio mikoa ya pembezoni.”

Alisema Serikali imepanga kutanua huduma hizo ili ziweze kutolewa katika hospitali zote za rufaa za mikoa, ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo imeanza kwa hospitali za rufaa za mikoa ya minane ambazo ni Bombo-Tanga, Meru-Arusha, Mtwara, Iringa, Bukoba-Kagera, Maweni-Kigoma na Sekoutoure-Mwanza.

Waziri Ummy alisema uanzishwaji wa kituo kimoja cha kutolea huduma ya kuchujia damu hadi kuanza kufanya kazi kama kilivyo cha Bombo kinagharimu sh milioni 574,794,177, hivyo kwa vituo hivyo nane ambavyo mwezi huu vinataanza kutoa huduma vitagharimu sh. bilioni 4.5.

Kwa upande wao,wagonjwa wenye matatizo ya figo waliishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma ya kuchuja damu katika hositali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga kwa kuwa awali walilazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo katika hospitali ya Muhimbili.

Pia, Wagonjwa hao licha ya kuishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma, pia wameiomba iangalie uwezekano wa kupunguza gharama ili watu wengi waweze kumudu matibabu hayo kwani kwa sasa gharama ya session moja ni sh. 250,000.

No comments:

Post a Comment