Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoka kwenye jengo la Kituo cha Pamoja cha Huduma za Fordha cha Horohoro mkoani Tanga wakati alipokitembelea kituo hicho, Machi 2, 2020. Kulia kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kituo cha dharura cha kuwapokea na kuwafanyia uchunguzi watu wanaoingia nchini kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga ambao wataonyesha kuwa na dalili za kuumwa magonjwa ya kuambukiza. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wa pili kushoto ni Naibu Waziri Nchi, Ofisi y Rais TAMISEMI, Mwita Waitara. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Mkinga, Danstan Kitandula wakati alipofungua jengo la Ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Mkinga na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo, Machi 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kufungua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Machi 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri. Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro, Tanga ambacho ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 7.6.
“Jengo hili kuta tayari zimeshaanza kuvimba, kwa nini majengo ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) yanajengwa kwa kiwango cha chini na kwa nini mmeruhusu majengo haya yatumike,” amehoji Waziri Mkuu.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amemtaka Afisa Miliki wa TRA, Bw. Haruna Sumwa, mkandarasi aliyejenga jengo hilo pamoja na wote waliohusika na ujenzi huo wafike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Machi 11, 2020.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. Amesema ni lazima majengo hayo yakidhi viwango.
“Hapa ni sura ya nchi ni lazima majengo yawe katika hali nzuri, haiwezekani mgeni anaingia na kuhudumiwa katika jengo chakavu, tutachukua hatua kwa yeyote aliyehusika, hizi ni fedha za umma lazima zitumike vizuri.”
Awali, Mkuu wa wilaya ya Mkinga Bw Yona Maki alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza Julai 2011 hadi Septemba 2014 na lilianza kutumika Agosti 2015 likiwa na taasisi 16 za Serikali zinazofanyakazi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nyumba 62 za watumishi, maji safi na salama pamoja na upungufu wa watumishi.
Majukumu ya kituo hicho ni pamoja na kusimamia, kudhibiti uingiaji na utokaji wa raia wa Tanzania na wageni, kufanya doria na misako hasa kwenye vipenyo ambako wale wasiopenda kufuata taratibu hupenda kutumia.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza watu wote wanaoingia nchini kupitia mipaka mbalimbali wapimwe afya zao ili kulikinga Taifa na maambuki ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.
Pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano na Serikali kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu. “Lazima tulinde nchi yetu katika kupambana na kuzuia magonjwa mbalimbali kwa kuhakikisha watu wote wanaingia nchini wawe salama.”
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga kuimarisha doria katika maeneo ya mpakani ikiwa ni pamoja na kukagua maroli kwa kuwa yanahusika na ubebaji wa wahamiaji haramu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kutojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuwa madhara yake ni makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema wananchi wakatae kutumika katika kupitisha dawa za kulevya na atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. “Usikubali gari lako likatumika kubeba wahamiaji haramu wala dawa za kulevya kwani ukikamatwa linataifishwa.”
Waziri Mkuu amesema mwaka jana dawa za kulevya aina ya heroine gramu 746, bangi kilo 485, mirungi kilo 880 zilipitishwa katika wilaya hiyo kiawango ambacho ni kikubwa, hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya aimarishe doria.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alitaja changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ikiwemo ya ukosefu wa maji safi na salama, ambapo Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imeshaanza kushughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment