Mwenyekiti wa Mkutano wa Kamati ya Watalaam na Makamishna wa
masuala ya nishati kutoka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye pia ni Kamishna wa Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati(Tanzania), Adam Zuberi,( kulia) akizungumza na wajumbe wa mkutano huo( hawapo pichani) wakati akifunga mkutano huo uliofanyika jijijini Dar Es Salaam kwa siku nne, Februari 25-28, 2020.
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati( Tanzania),Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Edward Ishengoma( CERE)( kushoto),Kamishna Msaidizi wa Umeme( ACE), Mhandisi Innocent Luoga( kulia) na Mhandisi Joyce Kisamo, wakifuatilia mada wakati wa ufungaji wa mkutano wa Wataalamu wa Masuala ya Nishati wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) uliofanyika Jijijni Dar Es Salaam Februari 25 - 28, 2020.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Wataalamu wa Masuala ya Nishati wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) uliofanyika Jijijni Dar Es Salaam Februari 25 - 28, 020 wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Maendeleo ya umeme, Mhandisi Styden Rwebangila (katikati) baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Mkutano wa Kamati ya Watalaam na Makamishna wa masuala ya nishati kutoka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), ambaye pia ni Kamishna wa Mafuta na Gesi, Wizara ya Nishati, Tanzania, Adam Zuberi,( kulia) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga mkutano wa Wataalamu wa Masuala ya Nishati wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) uliofanyika Jijijni Dar Es Salaam, Februari 25 - 28, 2020.
Mwenyekiti wa Mkutano wa Watalaamu na Makamishina masuala ya Nishati kutoka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), ambaye pia ni Kamishna wa Mafuta ya Gesi kutoka Wizara ya Nishati(Tanzania), Adam Zuberi amesema mkutano huo umepitisha kwa
pamoja mapendekezo tisa yanayohusu masuala ya nishati katika nchi hizo.
Adam alisema, Mkutano huo ulifanyika kwa siku nne Jijijni Dar Es Salaam,umemalizika (leo) Februari 28, 2020 ambapo ulianza Februari 25,2020 kwa kuwakutanisha Watalaamu na Makamishna wa Nishati kutoka Nchi za SADC.
Alisema mapendekezo hayo waliyokubaliana yatakabidhiwa kwa Makatibu Wakuu husika na baadaye kuwasilishwa katika mkutano wa Mawaziri wa masuala ya nishati kwa nchi za SADC unaotarajia kufanyika mwezi Mei mwaka huu ili kuyatolea maamuzi.
Wakati akifunga mkutano huo, Zuberi alitaja baadhi ya mapendekezo yaliyopitishwa kuwa ni pamoja na kuanzisha Mpango Kabambe wa Matumizi bora ya gesi asilia katika nchi za SADC.
“Tayari kuna mshauri mwelekezi ameshaanza kazi hiyo, lakini pili tumeamua kila nchi iendelee kuhamasisha nchi nyingine ili kusaini uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha Kuendeleza Nishati Jadidifu na Matumizi bora ya Nishati kwa Nchi SADC SACREE ili utekelezaji wake uanze,” alisema Zuberi .
Mapendekezo mengine ni kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya nidhati kati ya nchi na nchi pamoja na uanzishwaji wa sera ya ushirikishaji wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, pendekezo ambalo limeshaanza baada ya kupatikana mshauri mwelekezi.
Vilevile alisema kuwa suala la uhamasishaji na utekelezaji wa pamoja wa matumizi bora ya Nishati Jadidifu pia lilijadiliwa kwa kina katika mkutano huo ambapo kila nchi wanachama walieleza umuhimu wake katika kulinda mazingira na kuhakikisha nchi zenye uhaba kutumia vyanzo hivyo kwa nishati bora.
“Kwa hiyo maeneo hayo yamejadiliwa kwa kina, mjadala ulikwenda vizuri na kamati ikakubaliana kuwasilisha mapendekezo hayo katika baraza la mawaziri lijalo,”amesema Zuberi.
Hata hivyo mkutano huo pia ulijadili mchakato wa uanzishaji wa Kituo cha Umahiri cha Kuendeleza Nishati Jadidifu na Matumizi bora ya Nishati kwa Nchi SADC (SACREE), mapitio ya Itifaki ya Nishati ya 1996.
Pia ulijadili utekelezaji wa Mpango Kabambe wa utekelezaji wa Matumizi ya Gesi asilia katika nchi za SADC pamoja na mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Sekta ya Nishati chini ya Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Miundombinu katika Mtangamano(RIDMP), utakaofikia tamati mwaka
2027.
Ikumbukwe kwamba Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Agosti 17 na 18,2019, jijini Dar Es Salaam na kukabidhi majukumu ya uongozi wa jumuiya hiyo kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada ya Rais wa Namibia, Hage Geingob kumaliza muda wake.
Hivyo katika mkutano 40 wa jumuia hiyo utakaofanyika nchini Msumbiji, Tanzania itakabidhi kijiti cha majukumu ya uongozi wa jumuiya hiyo kwa Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi baada ya Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe kumaliza muda wake.
No comments:
Post a Comment