Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa ofisi yake kilichofanyika Februari 3, 2020 Jijini Dodoma , kushoto kwake ni Mwenyekiti wa baraza hili Bw. Tixon Nzunda ambaye ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu na Bunge , na kulia ni katibu wa baraza hilo Bw. Paschal Vyagusa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakati wa kikao chao cha kwanza cha mwaka kilichofanyika Februari 3, 2020 Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi hiyo Bw. Tixon Nzunda kushoto kwake waliokaa, na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Anthelmu Tarimo (kulia kwa waziri) pamoja na katibu wa baraza hilo Bw. Paschal Vyagusa wa kwanza kushoto waliokaa, wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza mara baada ya kikao hicho kufunguliwa rasmi Jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,
Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama
amewaasa watumishi wa Ofisi yake kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za
utumishi wa umma katika utendaji kazi wao ili kuendelea kuitumikia nchi kwa
weledi na ufanisi na kufikia malengo kwa wakati unaostahili.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kwanza cha mwaka
cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichofanyika Februari 3, 2020 Jijini
Dodoma.
Waziri Mhagama aliwataka watendaji wote kuona umuhimu wa
kuendelea kufanya kazi kwa weledi huku wakizingatia sheria za utumishi wa umma
ikiwemo nidhamu kazini, kauli nzuri kwa wateja, kuzingatia mavazi ya staha na
kuwahi kazini.
Waziri aliongezea kuwa, ni lazima mtumishi wa umma afanane na
kanuni na sheria za kiutimishi kwa kuwa na maadili mazuri awapo kazini na nje
ya kazi ili kujipatia sifa njema kuanzia muonekano hadi tabia kwa ujumla.
“Hatutegemei mtumishi wa umma tena wa ofisi hii anakuwa ndiye
mlevi wa kupindukia yaani ndiye namba moja Dodoma hii , wala kuvaa mavazi
yasiyoendana na hadhi ya utumishi wa umma, hiyo kwetu hatutoivumilia lazima
tuikatae na kuhakikisha tunakuwa mfano wa kuingwa,”Alisistiza
Waziri aliwakumbusha watendaji wa ofisi hiyo kuzingatia nafasi
zao za kiutendaji wawapo kazini kwa kuzingatia jukumu la ofisi yake ni Kuratibu
Shughuli zote za Serikali hivyo lazima iwe ofisi ya mfano.
“Ofisi yetu inaratibu shughuli zote za Serikali , muone ni kwa
namna gani sisi ni viungo kwa Serikali hii hivyo mtumie fursa ya baraza hili
kukumbushana wajibu wetu kwa kuhakikisha mnatekeleza majukumu kwa
nidhamu ya hali ya juu sana,”alisema Waziri Mhagama
Aliutaka uongozi pia kuendelea kuwa na umoja na kufanya kazi kwa
kuzingatia dhana ya ushirikishwaji ili kujenga tija kwa kupitia vikao ambavyo
vitaibua changamoto zinazowakabili pamoja na kuishauri vyema Serikali kuhusu
usimamizi wa kazi na rasilimali watu tunayoisimamia kila siku.
“Ni muhimu kuwa na vikao ili kuendelea kusimamia ustawi sehemu
zetu za kazi, na uwepo wa mabaraza haya utaleta tija kwa kuzingatia mchango
wake kwa Serikali nzima na hakikisheni mnayatumia kwa kuzingatia dhana ya
ushirikishaji,”alieleza Waziri
Aidha aliongezea kuwa ni muhimu viongozi wote kuanzia ngazi ya
Vitengo, Idara na Taasisi zote kuendelea kusimamia utekeleaji wa majukumu kwa
kufuata sheria, miongozo na kanununi za utumishi wa umma huku wakiwa na upendo
kati yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Tixon Nzunda
aliahidi na kumhakikishia Waziri kuwa, watatekeleza maagizo na maelekezo
aliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili mazuri na kuahidi kuendelea
kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo juu ya utoaji wa huduma bora
inayozingatia viwango vya hali ya juu.
“Tunakushukuru Waziri na nikuhakikishie kuwa unatimu imara,
tulivu na chapakazi na tutatekeleza maagizo yote kwa kasi ya mabadiliko ya hali
ya juu,”alisema Bw.Tixon
Naye mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Bi. Numpe Mwambeja alieleza
furaha yake kwa kumshukuru Waziri kwa maelekezo yake yenye nia njema ya
kuendelea kuona ofisi yake inakuwa ya mfano katika utendaji kazi wa kila siku
na kuahidi kuzingatia maagizo aliyoyatoa.
“Kwa niaba ya wajumbe wenzangu wa kikao cha baraza
nimefarijika sana na maagizo yaliyotolewa na waziri ikiwemo kuzingatia suala la
uadilifu, kuwahi kazini, kuvaa mavazi ya staha, kuacha uvivu na kuwa na kauli
nzuri katika hudumia wateja wa ndani na nje ya ofisi ili kufanya kazi zetu kwa
ufanisi unaotakiwa,”alisema Bi. Numpe.
=MWISHO=
No comments:
Post a Comment