Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Capt. Mstaafu George Mkuchika akimpongeza mkazi wa kijiji ya Inzovu wilayani
Mpwapwa mkoani Dodoma Bw.Yohana Yaredi
Mogoile kabla ya kumkabidhi hatimilki ya
kimila ya kumiliki ardhi mkazi huyo wakati wa hafla ya kukabidhi hati hizo baada
ya zoezi la urasimishaji ardhi kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), hayo yamejiri Januari 1, 2020.
Naibu
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Dkt. Mary Mwanjelwa akisisitiza umuhimu
wa elimu kuhusu urasimishaji ardhi na faida zake kwa wananchi Wilayani Mpwapwa
wakati wa hafla ya utoaji hati milki za kimila za kumiliki ardhi, baada ya
zoezi la urasimishaji ardhi kupitia
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA)na
Halmashauri ya wilaya hiyo, hayo
yamejiri Januari 1, 2020 ambapo Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt.
Mstaafu George Mkuchika alikuwa mgeni
rasmi.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Kapt. mstaafu George Mkuchika akiwa kwenye picha ya pamoja na wananchi wa kijiji
cha Inzovu wilayani Mpwapwa mkoani
Dodoma waliopatiwa hatimilki za kimila za kumiliki ardhi katika Kijiji hicho baada ya kurasimisha
mashamba yao.
Na Mwandishi Wetu
Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia Mpango
wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za
Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Inzovu wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wakati akikabidhi hati kwa wananchi
walinufaika na mpango huo, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa dhamira
ya Serikali kupitia mpango huo ni kuwawezesha wananchi kupitia hatimilki za
kimila za kumiliki ardhi wanazopatiwa baada ya kurasimisha mashamba yao.
“ Mabenki yametuhakikishia kuwa
yanawakopesha wananchi kupitia hatimilki za kimila za kumiliki ardhi
zinazotolewa kwa wananchi baada ya kurasimisha mashamba yao kwa kuyapima na
hivyo kuweza kujenga uwezo wa kujikwamua kiuchumi, wafanyabiashara wote wakubwa
na wenye maduka wanakopa katika taasisi za fedha hivyo waliopata hati hizi
zitumieni kujiletea maendeleo”, alisisitiza Waziri Mkuchika.
Akifafanua amesema kuwa kuwepo kwa
MKURABITA ni matokeo ya sera nzuri za Chama cha Mapinduzi zinazoelekeza katika
kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi hasa wanyonge kwa kutumia rasilimali
zilizopo katika maeneo yao ikiwemo ardhi.
Akitaja faida za urasimishaji ardhi
Waziri Mkuchika amesema kuwa ni pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi na
kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mratibu wa
MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema
kuwa mashamba 707 yalipimwa katika kijiji cha Inzovu huku 593 yakiwa ndiyo
yenye sifa za kupatiwa hati milki za kimila za kumiliki ardhi.
“ Hati 159 zimeshaandaliwa na kutolewa
kwa wananchi waliopo hapa na zilizobaki 434 tutahakikisha zinaandaliwa na
zinawafikia walengwa kwa wakati tukishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Mpwapwa,s” alisisitiza Dkt. Mgembe
Akifafanua, Dkt. Mgembe amesema kuwa
MKURABITA itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo katika kuwajengea uwezo
wananchi wote walionufaika na urasimishaji ili waweze kutumia hati walizopata
kujiletea maendeleo kupitia mafunzo yatakayoendeshwa kwa kushirikiana na taasisi
za fedha yakiwemo mabenki na Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Aidha, Dkt. Mgembe aliahidi kuwa
MKURABITA itahakikisha kuwa inajenga masjala ya kutunza hati katika kijiji
hicho na kuwaasa wananchi kujitolea kushiriki katika kufanikisha kazi hiyo
kupitia nguvu kazi yao.
Katika kuunga mkono jitihada za
Serikali kuwawezesha wananchi Benki ya CRDB, TPB na NMB zimekuwa zikiwakopesha
wananchi wenye hatimilki za kimila ili waweze kujiletea maendeleo na hivyo
kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mwisho
No comments:
Post a Comment