Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe (Mb) akijibu swali bungeni
Jijini Dodoma leo tarehe 3 Februari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane.
Na Mathias Canal,
Wizara ya kilimo-Dodoma
Serikali
imewahakikishia wakulima wa Pamba nchini kuwa itaendelea kufuatilia upatikanaji
wa viuadudu vya zao la pamba na kuhakikisha vinawafikia wakulima kwa wakati.
Naibu Waziri wa Kilimo
Mhe Hussein Bashe ameyasema hayo tarehe 3 Februari 2020 wakati akijibu swali la swali la Mbunge wa Jimbo la Geita
Vijijini Mhe Joseph Kasheku Msukuma aliyetaka kufahamu serikali inampango gani
kupeleka dawa za kuuwa wadudu wa Pamba kwani zinazopatikana huwa ni chache.
Bashe amesema kuwa kama
sehemu ya utekelezaji wa hamasa za kilimo cha Pamba, katika msimu wa kilimo wa
mwaka 2017/2018 eneo la ekari 1,488,406 lililimwa
na kuzalisha kiasi cha tani 132,961. Chupa milioni 4.6 za viuadudu zenye thamani ya shilingi bilioni
16.8 na vinyunyizi 15,300 vyenye thamni ya shillingi milioni 462 vilinunuliwa
na kusambazwa mwaka huo.
Aidha, katika msimu wa
2018/2019 eneo la ekari 1,865,000 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 222,725
ambapo chupa milioni 6 za viuadudu
vyenye thamani ya shilingi bilioni 29 na vinyunyizi 23,000 vyenye thamani ya
shilling bilioni 1.8 vilinunuliwa.
Vilevile, katika msimu
wa 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani
350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya shilingi bilioni 41 na
vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6 vilinunuliwa.
Mhe Bashe amesema kuwa katika
msimu wa 2017/2018 jumla ya ekapaki 965,300 na vinyunyizi 3,302 vilisambazwa
katika Mkoa wa Geita. Aidha, jumla ya ekapaki 736,345 na vinyunyizi 3,020
vilisambazwa katika mkoa huo katika msimu wa 2018/2019. Kwa msimu wa 2019/2020
Mkoa wa Geita umekwisha kusambaziwa kiasi cha ekapaki 8,748 na usambazaji bado
unaendelea.
Bashe amesema, si
sahihi kusema kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha pamba ikiwa haina uwezo wa kupeleka sumu za kuulia
wadudu na hata zinapopatikana huwa ni
chache. Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao likiwemo zao la pamba
ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akizungumzia uchache wa
viuadudu vya zao la pamba Mhe Bashe amesema kuwa umechangiwa na baadhi ya
wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine kama vile mahindi na
viazi vitamu ili kudhibiti viwavijeshi vamizi.
Vilevile, amesema kuwa kukosekana
kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika baadhi ya maeneo ukiwemo
Mkoa wa Geita ambapo viuadudu havikupelekwa kwa wakulima na badala yake kuuzwa
katika maduka ya pembejeo kinyume na taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao
la pamba.
Ameongeza kuwa Watu zaidi ya
12 walikamatwa na kati yao 9 walifunguliwa mashtaka ambapo watu nane (8)
walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja.
MWISHO
No comments:
Post a Comment