Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akijibu maswali Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 3 Februari 2020.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet
Hasunga (Mb) ameliarifu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mazao
yote ya kimkakati yanasimamiwa na Bodi za Mazao husika sio vyama vya Ushirika.
Mhe Hasunga ameyasema hayo leo
tarehe 3 Februari 2020 wakati akijibu maswali Bungeni ambapo amesisitiza kuwa
vyama vya Ushirika vina jukumu la kukusanya mazao na kuyapeleka sokoni kwa
ajili ya kuuza kwa niaba ya wanachama sio kusimamia uzalishaji.
Amesema kuwa jambo hilo
litaendelea vivyo hivyo na kuwekewa mkakati wa kuimarishwa zaidi ili kuwasaidia
wakulima kunufaika na kipato kinachotokana na tija katika uzalishaji wa mazao
nchini.
“Tunataka mazao yote,
pembejeo zote kuanzia (mbegu, mbolea, viuadudu) hivi vyote vitakuwa
vinasambazwa na sekta binafsi katika maeneo yote sio serikali” Alikaririwa Mhe
Hasunga
Kadhalika, amewataka
wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo ya kuuza viuatilifu kwani serikali
inaendelea kuruhusu sekta binafsi kupeleka viuadudu kwenye mazao mbalimbali
kama vile Korosho, Pamba, Kahawa na mazao mengine yote.
Ameongeza kuwa jukumu la
serikali itakuwa ni kusimamia na kuratibu maendeleo ya mazao husika na namna ya
kutafuta masoko lakini sio kusambaza pembejeo.
Mhe Hasunga amesema kuwa hiyo
ni fursa kwa watanzania wote wanaotaka kufanya biashara hiyo kujitokeza kwa
wingi.
Waziri Hasunga amesema kuwa
baadhi ya viongozi wa vyama vya Ushirika waliingia kwenye biashara ya Tumbaku
na kuuza zao hilo bila kufuata utaratibu hivyo kuathiri bei ambayo ingetokana
na soko.
Amesema Kutokana na
changamoto hiyo Wizara ya kilimo ilikabidhi taarifa ya uchunguzi kwenye uongozi
wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuwachukulia hatua
viongozi wote waliokiuka maadili ya uongozi na wale ambao hawakusimamia mazao
ipasavyo hivyo kusababisha hasara kwa wananchi na vyama vya Ushirika.
Zoezi hilo linaendelea nchi
nzima kwani viongozi husika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwemo kurejesha
fedha walizopora.
MWISHO
No comments:
Post a Comment