Sunday, February 2, 2020

MHE BASHUNGWA AUNGANA NA WAFANYABIASHARA WADOGO, ATAKA BRAND YA "UJI WA MAMA REGINA" ITAMBULIKE


 Na Mathias Canal, Wazo Huru Blog, Dodoma

Tarehe 17 Machi, 2018 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilizindua utoaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na Wamachinga. Utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara hao unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 yaliyofanywa na Kikao cha Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

Zoezi hili lilipaswa kutekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji.

Lakini Disemba 10, 2018 Mhe Rais John Magufuli alilazimika kuingilia kati na kutoa vitambulisho maalum 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania kwaajili ya kuwagawia wajasiriamali katika mikoa yao wakiwemo wa machinga vitakavyouzwa kwa Sh20,000 kwa kila kimoja ikiwa ni baada ya kuona mamlaka zenye jukumu hilo zinachelewa huku wafanyabiashara wakiendelea kusumbuliwa.

Kama ilivyo kawaida kwa wafanyabiashara wadogo nchini huitwa wadogo kwa kuwa mtaji wao hauvuki Milioni 4 japo wapo pia wenye mtaji wa chini ya Tsh 10000.

Dada Regina S. Majengo yeye ni mkazi wa Jiji la Dodoma ambaye amejikita katika biashara ya kuuza uji ambayo mtaji wake hauzidi Tsh 17,000 lakini aliitikia mwito wa serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ya kuwa na kitambulisho cha ujasiriamali.

Akiwa pembezoni mwa mgahawa mmoja maarufu KAHAWA CAFE Jijini Dodoma tarehe 2 Februari 2020 Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa amekutana na Dada Regina Majengo ambaye kama lengo la wateja wengine ni kununua uji ambaye alimuhakikishia Waziri huyo kuwa biashara hiyo ndio inamfanya kuendesha maisha kwa uhuru na amani. 

Mhe Bashungwa amechukua hatua za haraka ambapo amewasiliana na wamiliki wa Mgahawa mpya wa Kahawa Cafe Jijini Dodoma kuona kama kwenye menu yao ya wanaweza kuweka uji kwa brand ya mama ijulikanayo kama “Uji Mama Regina” ili kumsaidia mama huyo lakini kufungamanisha mafanikio yao na wafanyabiashara wadogo ambao nao pia wana ndoto za kukua kibiashara.

Katika hatua za awali,  mmiliki wa mgahawa huo amekubali ombi hilo la Waziri Bashungwa ambao alimuita Regina kupanga namna "UJI MAMA REGINA" utakavyokuwa sehemu ya Menu ya mgahawa. 

Akizungumza na Tovuti ya Wazo Huru Mhe Bashungwa amesema kuwa wizara yake inaendelea kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo nchini ili kuimarisha sekta hiyo na kukuza wafanyabiashara wengi nchini.

Pamoja na mambo mengine Waziri Bashungwa amempongeza mama Regina kwa kuwa na kitambulisho cha biashara huku akiwasihi wafanyabiashara wengine wadogo kote nchini kuhakikisha kuwa wanakuwa na vitambulisho hivyo ili waweze kutambulika.

MWISHO

No comments:

Post a Comment