Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akisisitiza umuhimu wa Tathmini ya Uharibifu na Mahitaji Baada ya Maafa kutokea, Jijini Tanga, wakati alipofungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wanaohusika na Tathmini ambayo huainisha madhara, hasara za kiuchumi, na gharama za mahitaji ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea..Kulia ni Katibu Tawala wa mkoa huo Noel Kazimoto
Baadhi ya wataalamu wa menejimenti ya maafa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa Tathmini ya Uharibifu na Mahitaji Baada ya Maafa kutokea, kabla ya kufanya tathmini hiyo katika Halmashauri za mkoa wa Tanga. Tathmini huainisha madhara, hasara za kiuchumi, na gharama za mahitaji ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Mratibu kutoka Benki ya Dunia, Nyambiri Kimacha akisisitiza umuhimu wa Tathmini ya Uharibifu na Mahitaji Baada ya Maafa kutokea, Jijini Tanga, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wanaohusika na Tathmini kabla ya kufanya tathmini hiyo ambayo huainisha madhara, hasara za kiuchumi, na gharama za mahitaji ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Tathmini ya Uharibifu na Mahitaji Baada ya Maafa, ni mfumo wa kimataifa uliokubaliwa kuainisha madhara, hasara za kiuchumi, na gharama za mahitaji ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea. Mfumo huo hutumiwa na mataifa mengi duniani katika kuainisha athari hizo kwa kuzingatia aina ya maafa wanayoyapata, ambapo serikali hutambua ni kwa kiwango gani maafa yamekuwa yakiathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na pato la taifa na hivyo kuweka mikakati thabiti ya kuzuia na kupunguza madhara.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya menejimenti ya maafa imeratibu zoezi la kufanya tathmini kwa kutumia mfumo huo kwa mara ya kwanza hapa nchini mkoani Tanga kwa kuwa mkoa huo ni miongoni mwa mikoa iliyopata maafa ya mafuriko na kupata madhara makubwa katika sekta za Kilimo, Afya, Elimu, Mazingira na Miundombinu kufuatia athari ya mvua za vuli za mwezi Oktoba hadi Desemba, mwaka jana (2019).
Akiongea wakati wa kufuatilia uratibu wa tathmini hiyo jijini Tanga, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amefafanua kuwa Serikali kwa kushirkiana na benki ya dunia mwaka jana walitoa mafunzo kwa watalaam wa sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kitaalamu wa kufanya tathmini hiyo na kwa sasa wanafanya tathmini kwa vitendo mkoami humo, lengo ni kuwa na wataalamu wenye uwezo huo kuanzia ngazi za msingi za menejimenti ya maafa.
“Mfumo huu utatusaidia kupata taarifa ya kina ya madhara, matokeo na rasilimali zinazohitajika katika kurejesha hali kwa kila sekta iliyoathiriwa, pia taarifa zake zinasaidia kuandaa mkakati wa kitaifa na wa kimkoa wa kurejesha hali na hatimaye Kuweka mfumo wa Kitaifa na kimkoa wa kurejesha hali kwa kipindi cha sasa na baadaye.”Amesisitiza Kanali, Matamwe.
Kanali Matamwe, amefafanua kuwa Tathmini hiyo ni shirikikshi kwa maana ya sekta ya umma na sekta binafsi ambapo wadau wa masuala ya maafa hushirikishwa yakiwemo mashirika ya umoja wa mataifa, Benki ya dunia na Mashirika yasiyo ya kiserikali. Aidha, ameeleza kuwa zoezi hilo linalenga kujenga uwezo kwa vitendo kwa wataalamu kutoka katika ngazi ya wizara, mkoa na wilaya katika kufanya tathmini ya uharibifu na mahitaji kutokana na maafa kwa kila sekta.
Naye mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa, kwa mujibu wa sheria ya Maafa Na.7 ya mwaka 2015, ambaye ni Katibu Tawala wa mkoa, akiwakilishwa na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto amefafanua kuwa mkoa huo mvua za msimu uliopita wa vuli wa mwaka jana, mkoa huo ulipata athari zinazojumuisha vifo, uharibifu wa miundombinu ya barabara, maji, na miundombinu ya kutolea huduma za elimu na afya, pia kubomoka kwa makazi na kuharibika kwa mfumo wa maisha ya kijamii ya kila siku.
Aidha, ameongeza kuwa, Tathmini hiyo itaujengea uwezo mkoa huo kuandaa mipango na mikakti ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu katika kurejesha hali katika ubora zaidi, kwa kuwa imejikita katika kuangalia madhara yaliyojitokeza katika sekta ya elimu, afya, kilimo, makazi, miundombinu pamoja na huduma za maji na usafi. Vilevile tathmini hiyo imeangalia masuala mtambuka, kama vile mazingira, masuala ya upunguzaji wa athari za maafa na usawa wa kijinsia.
Tathmini hiyo iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia, kwa kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa chini ya Uongozi wa mtaalam mshauri kutoka nchini Ghana Seth Vordzorgbe, imewahusisha wataalamu kutoka katika ngazi ya wizara, mkoa na wilaya pamoja na wadau wa sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
No comments:
Post a Comment