Tuesday, February 18, 2020

ASKARI WAASWA KUEPUKA VITENDO VINAVYOLITIA DOSARI JESHI LA POLISI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na askari wa Jeshi la Polisi mkoani humo katika kikao kilichofanyika Februari 17, 2020 Mjini Bariadi.Baadhi ya askari Polisi mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka katika kikao kilichofanyika  Februari 17, 2020 Mjini Bariadi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, SACP Henry Mwaibambe akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kulia) azungumze na askari wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa katika kikao kilichofanyika Februari 17, 2020 Mjini Bariadi.
Askari wa Jeshi la Polisi, Koplo Abdallah Manzi akichangia hoja katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na askari hao, kilichofanyika  Februari 17, 2020 Mjini Bariadi.
Askari mkoani Simiyu wameaswa kulinda hadhi ya jeshi la polisi kwa kujiepusha na vitendo viovu vinavyolitia dosari jeshi hilo.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akizungumza na askari polisi wa mkoa huo Februari 17, 2020 ambapo amevitaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kutoa siri za jeshi, kuomba rushwa, utapeli na kushiriki kuharibu ushahidi katika baadhi ya kesi.

“Ni jambo la aibu kwa askari kushiriki katika uhalifu,  kutoa siri za jeshi na kugeuka kuwa mtoa taarifa kwa wahalifu, ipendeni kazi yenu muepuke mambo yanayodhalilisha jeshi na mjenge tabia ya kuonyana ili mlinde heshima ya jeshi letu,” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka ametoa wito kwa askari polisi mkoani Simiyu kujiendeleza kielimu ili waweze kupata sifa za kulitumikia jeshi katika nafasi mbalimbali huku akiwaeleza umuhimu wa kujenga makazi na kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo Mkoani humo kwa lengo la kutengeneza kipato cha zaida.

Katika hatua nyingine  Mtaka ametoa wito kwa viongozi wa Jeshi la Polisi kutenda haki kwa askari walio chini yao, ikiwemo kutoa nafasi ya kuwapandisha vyeo askari wanaostahili  kwa wakati uliopo ili kuwapa motisha katika kazi yao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, SACP Henry Mwaibambe amesema kuwa katika Awamu hii ya tano hakuna kisingizio kwa askari kutofuata taratibu katika utendaji kazi wao.

“Zamani ilikuwa siyo rahisi sana kumkamata tajiri , lakini sasa hivi Watanzania wote tuko (level) hali moja hakuna cha huyu ni nani na yule ni nani; sasa hivi mtu asipofuata taratibu ni mapungufu yake binafsi ; tunafanya kazi kwa kufuata taratibu za jeshi pasipo kuingiliwa na mtu yeyote nje ya taratibu za jeshi, sisi tuliokaa muda mrefu kwenye jeshi la Polisi tunajua kazi nzuri inayofanywa na Mhe. Rais,” alisema Mwaibambe.

Mwaibambe ameongeza kuwa askari kama watumishi wa umma wengine wanapaswa kujiepusha na masuala yanayoleta malalamiko kwa wananchi huku akisisitiza kuwa hawatasita kuwachukulia hatua askari watakaoshindwa kufanya kazi kwa uadilifu.

Kwa upande wao askari wamesema watafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu huku wakiomba Serikali ya Mkoa iweze kuwasaidia upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya kujenga makazi yao binafsi na maeneo ya kuweka uwekezaji wao.

“Mhe. Mkuu wa Mkoa umezungumza suala la Askari kujenga makazi, tunaomba Serikali ya mkoa ione namna ya kutusaidia kupata viwanja vya makazi katika maeneo yaliyopimwa na Halmashauri kwa gharama nafuu ili tuweze kujenga maana tunatamani kujenga Simiyu,” alisema Koplo Abdallah Manzi.

No comments:

Post a Comment