Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akisalimiana na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe. Roberto Mengoni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais, Mtaa wa Luthuli Dar es Salaam. Mazungumzo baina yao yamejikita katika nyanja za kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akizungumza na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe. Roberto Mengoni katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais Luthuli Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, nchi hizi mbili zimekubaliana mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu pamoja na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe. Roberto Mengoni wakiwa katika kikao cha pamoja, (katikati) ni Bi. Haikael Shishira na Kisa Mwaseba maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bi. Kemilembe Mutasa, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Zungu
amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kuendeleza mashirikiano na Serikali ya Italia
katika nyanja za Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Hayo ameyasema hii leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya mazungumzo na
Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni katika Ofisi ndogo ya Makamu wa
Rais Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam.
Amesema suala la Mabadiliko ya Tabianchi ni changamoto kubwa duniani kwa hivi sasa
na nchi zinazoendelea ndio waathirika wakubwa kutokana na uchafuzi wa mazingira
unaofanywa na nchi zilizoendelea.
Waziri Zungu ametoa wito kwa Serikali ya Italia kuendeleza mashirikiano katika nyanja
za udhibiti wa taka na kujenga uwezo katika uzalishaji wa nishati mbadala ili kukabiliana
na uharibufu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na
Mkaa.
“Serikali ya Rais John Joseph Pombe Magufuli inatekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa
kufua Umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji kwa lengo la kuongeza nishati ya
Umeme na kukuza sekta ya viwanda nchini” Zungu alisisitiza.
Asema kukamilika kwa mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere utachochea
jitihada za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira utokanao na ukataji wa miti
kwa matumizi ya nishati ya kupikia. Ameongeza kusema kuwa jitahada za dhati
zinatakiwa kuwepo pia katika uzalishaji wa umeme wa nishati ya jua na upepo.
Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Tanzania amesema kuwa nchi yake inalenga
kutoa msukumo zaidi katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya Tabianchi,
kuhimiza kilimo rafiki kwa mazingira, nishati mbadala na nishati jadidifu.
Waziri Zungu amemuhakikishia Balozi Roberto ushirikiano wa dhati katika kupambana
na uharibufu wa mazingira nchini ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwa taifa la
sasa na vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment