Thursday, December 5, 2019

WAZIRI HASUNGA KUTENGUA UONGOZI WA WAKALA WA MBEGU UKISHINDWA KUZALISHA TANI 5000 ZA MBEGU MSIMU WA 2019/2020

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizindua matrekta matatu yaliyonunuliwa na Wakala wa Mbegu (ASA) kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa uzalishaji mbegu bora wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikabidhi mbegu Bora zilizozalishwa na Wakala wa Mbegu (ASA) kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa mazao Visiwani Zanzibar wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mbegu bora zilizozalishwa na Wakala wa Mbegu (ASA) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mbegu zinazozalishwa na Wakala wa Mbegu (ASA) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikata utepe kuashiria uzinduazi wa matrekta matatu yaliyonunuliwa na Wakala wa Mbegu (ASA) kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa uzalishaji mbegu bora wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametangaza kuifuta Bodi ya Wakala wa Mbegu (ASA) endapo itashindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu za kilimo zipatazo Tani 5000 katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.

Ametoa kauli hiyo jana tarehe 4 Disemba 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Taasisi hiyo mara baada ya kutembelea Mkoani Morogoro akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja ambapo amesema kuwa tishio hilo litahusisha pia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu.

Amesema kuwa pamoja na ASA kuongeza eneo la uzalishaji wa mbegu kutoka hekta 9890 mpaka kufikia hekta 10,115.2 lakini bado uzalishaji ni mdogo kwani ASA inazalisha Tani 1440 pekee huku zaidi ya asilimia 85 ya watanzania wanaojihusiaha na kilimo wakiwa na uhitaji wa mbegu.

Waziri Hasunga amesema kuwa matrekta matatu mapya yaliyonunuliwa na ASA pamoja na zana zake kama vile Boom Spayer, majembe matatu mapya na Planter tatu mpya yanapaswa kutumika ipasavyo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora.

“Sisi kama nchi tunahitaji Tani 100,086 za mbegu na mpaka sasa hivi uwezo wetu wa kuzalisha ndani na kuagiza nje hauzidi Tani 57,000 sasa mahitaji ni makubwa watu wanataka mbegu bora lakini uzalishaji bado upo chini” Amesisitiza Mhe Hasunga

Waziri Hasunga amesema kuwa mbegu bora ndio msingi na muhimili wa kilimo hivyo ili kubadilisha kilimo kutoka kujikimu na kuwa kilimo chenye tija na cha kibiashara ni lazima kuwa na uzalishaji mkubwa wa ndani ya nchi.

Aliongeza kuwa serikali itaiwezasha ASA kuongeza vituo vya usambazaji wa mbegu kutoka vitano ambavyo vinatumika sasa mpaka kuwa vituo 10 ili kuwarahisishia wakulima kupata mbegu katika maeneo yao.

Kadhalika, waziri Hasunga amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) kuhakikisha kuwa anatatua changamoto alizozibainisha kwenye taarifa yake ikiwemo ukosefu wa mtaji wa kutosha, kutokuwa na hifadhi ya mbegu ya Taifa, ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji, upungufu wa vitendea kazi na uhaba wa vituo vya kusambaza mbegu.

Changamoto zingine ni upungufu wa magari ya kusambaza mbegu, uchakavu wa mitambo ya kuchakata mbegu, na upungufu na uchakavu wa maghala ya kuhifadhia mbegu.

Wakala wa Mbegu (ASA) ulianzishwa chini ya sheria ya wakala za serikali sura ya 245 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kuzinduliwa rasmi tarehe 23 Juni, 2006 ikiwa ni Taasisi inayounganisha sekta ya umma na binafsi katika mfumo wa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora.

MWISHO

No comments:

Post a Comment