Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani, akizungumza na Wanachama wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kilimo na Masoko Mamsera leo Jumanne, Desemba 03, 2019 wilayani Rombo,mkoa wa Kilimanjaro.
Meneja wa Chama cha Ushirika cha Msingi Mamsera AMCOS, Mary Shayo akiwasilisha taarifa ya chama hicho kwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani leo Jumanne, Desemba 03, 2019 wilayani Rombo,mkoa wa Kilimanjaro.
Wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Mashati SACCOS wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani leo Jumanne, Desemba 03, 2019 wilayani Rombo,mkoa wa Kilimanjaro.
………………
Rombo,
Vyama vya Ushirika katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro vinakubalika kwa wananchi kutokana na huduma nzuri na shirikishi zinazotolewa kwa wanachama na viongozi wa Bodi za vyama hivyo kwa jamii nzima. Vyama hivi vimepata mafanikio mbalimbali tangu kuanzishwa kwake ikiwemo kuongezeka kwa mitaji pamoja na uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayowaingizia kipato wananchama wa vyama vya ushirika
Taarifa zilizotolewa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani, leo Jumanne, Desemba 03, 2019 wilayani Rombo, kwenye vyama vya ushirika alivyovitembelea zinaonyesha uwepo wa ongezeko kubwa la wanachama wanaojiunga na vyama vya ushirika ambavyo vimekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kujikwamua kiuchumi.
“Hali ya Ushirika niliyoiona na maendeleo yaliyopatikana katika vyama vya ushirika hapa Rombo imenipa faraja kubwa sana, kuwa kuna baadhi ya Watanzania bado wanauishi Ushirika , na ninawapongeza viongozi wa vyama hivi kwa kusimama imara katika kuvisimamia kwa kufuata Sheria na taratibu za Ushirika,” amesema Dkt. Kamani.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika anaeleza kuridhishwa na uendeshwaji wa vyama vya ushirika alivyovitembelea katika wilaya Rombo na kuvitaja kuwa Shamba Darasa la vyama vya msingi vinavyosimamiwa vizuri na kwamba popote atakapokwenda katika mikoa mbalimbali hapa nchini atawataka wanaushirika kuja Kilimanjaro katika wilaya ya Rombo kujifunza na kujionea mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia ushirika
Vyama vya ushirika ambavyo Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania amepata fursa ya kuvitembelea katika ziara yake ni pamoja na Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kilimo na Masoko Mamsera, Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Mashati na Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kilimo na Masoko Tarakea.
Meneja wa Chama cha Ushirika cha Msingi Mamsera AMCOS, Mary Shayo alisema idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 934 mwaka 1995 na kufikia wanachama 2,000 mwaka 2017/2018 na kwamba chama hicho kinahudumia wakulima zaidi ya 10,000.
Aidha, Mamsera AMCOS kimekuwa kikitoa gawio kila mwaka kwa wanachama wake na chama kimetenga mafungu kila mwaka kwa ajili ya kusomesha wanafunzi yatima na walio katika mazingira magumu ambapo mwanafunzi mmoja amesomeshwa hadi kuhitimu chuo kikuu (UDOM) na wengine wawili wamemaliza kidato cha nne huku wengine wanaendelea kusomeshwa pamoja na chama vilevile kimejenga jengo kubwa la kitega uchumi.
Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Mashati SACCOS kilianza na wanachama 17 mwaka 1987 na hivi sasa kina wanachama 3,511, Akiba za Wanachama Shilingi 3,101,832,070, Hisa za Wanachama Shilingi 225,318,000 na Amana za Wanachama Shilingi 45,131,552. Aidha, chama hicho kimewekeza fedha za hisa za Wanachama katika makampuni mbalimbali Zaidi ya Shilingi 234,439,552 na chama kimeweka Bondi Benki Kuu ya Shilingi 1,329,786,002 na Mtaji wa chama ni Shilingi 336,530,238.
Idadi ya Wanachama katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kilimo na Masoko Tarakea AMCOS wameongezeka kutoka 55 mwaka 1961 na kufikia wanachama 2,870 hivi sasa. Aidha, Chama kimeweza kujenga Ukumbi wa Mikutano na Ukuta kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chama bila kuchangisha mwanachama, gharama za ujenzi mpaka sasa imefikia Shilingi 197,349,701. Vilevile Chama kiliweza kuwalipia sehemu ya ada wanafunzi 12 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 12 kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijafuta ada kwenye shule za msingi na sekondari za Serikali.
No comments:
Post a Comment