Mwekezaji kutoka
nchini Uturuki, Bw. Mustafa Albayram akizungumza na baadhi ya viongozi
wa mkoa wa Simiyu wakati alipotembelea eneo la Isanga lililotengwa kwa
ajili ya uwekezaji wa Viwanda katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi
mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake ambayo amefuatana na Balozi wa
Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akisalimiana na
Mwekezaji kutoka nchini Uturuki Bw. Mustafa Albayram mara tu baada ya
kuwasili Mjini Bariadi Novemba 13, 2019 kwa ziara ya siku mbili yenye
lengo la kuangalia mazingira ya uwekezaji katika viwanda ambaye
amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth
Kiondo(katikati).
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bw. Jumanne Sagini akionesha moja ya eneo linalofaa kwa uwekezaji katika
Kata ya Nyakabindi Mjini Bariadi, wakati wa ziara ya Balozi wa Tanzania
nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo ambaye alifuatana na Mwekezaji
kutoka nchini Uturuki Bw. Mustafa Albayram mara tu baada ya kuwasili
Mjini Bariadi Novemba 13, 2019 kwa ziara ya siku mbili yenye lengo la
kuangalia mazingira ya uwekezaji katika viwanda.
Mwekezaji kutoka nchini Uturuki
Bw. Mustafa Albayram(kulia) akiwaonesha jambo Katibu Tawala wa Mkoa,
Bw. Jumanne Sagini na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kutoka
katika simu yake mara baada ya kutembelea eneo la Isanga lililotengwa
kwa ajili ya uwekezaji wa Viwanda katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi
mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake ambayo ameambatana na Balozi wa
Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bw.Jumanne Sagini(kushoto) akisalimiana na Mwekezaji kutoka nchini
Uturuki Bw. Mustafa Albayram mara tu baada ya kuwasili katika Uwanja wa
Ndege wa Mwanza Novemba 13, 2019 kwa ajili ya ziara ya siku mbili
mkoani Simiyu yenye lengo la kuangalia mazingira ya uwekezaji katika
viwanda ambaye amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof.
Elizabeth Kiondo(katikati)
*************************************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mwekezaji kutoka
nchini Uturuki, Bw. Mustafa Albayram ameahidi kujenga viwanda viwili;
kiwanda cha nguo na kiwanda cha kutengeneza glasi katika eneo la Isanga
Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mwaka 2020, mara baada ya kuridhishwa na
mazingira ya uwekezaji ambapo viwanda hivyo vinatarajia kuajiri
wananchi takribani 2000.
Albayram
ameyasema hayo Novemba 13, 2019 mara baada ya kutembelea maeneo
mbalimbali kwa lengo la kuangalia mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa
viwanda, ambaye alifuatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof.
Elizabeth Kiondo kwa ziara ya siku mbili mkoani Simiyu.
Amesema
endapo miundombinu yote muhimu hususani umeme itawekwa kwa wakati katika
eneo hilo uwekezaji huo utaanza mara tu baada ya kukamilisha taratibu
zote muhimu zinazohitajika ikiwa ni pamoja na usajili wa kampuni na
kutafuta hati miliki ya ardhi.
“Tumeamua
kuwekeza Simiyu, kila kitu kikienda sawa kiwanda cha nguo kinaweza
kujengwa na kufanya kazi ndani ya miezi tisa mpaka mwaka mmoja, kiwanda
cha glasi ni mwaka mmoja; baada ya usajili wa kampuni nitarudi tena
Simiyu kukamilisha masuala ya hati miliki ya ardhi, sitaki kumuangusha
Mhe. Balozi maana amefanya mengi kwa ajili yetu,” alisema Albayram.
Balozi wa
Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo amesema mwekezaji
ameridhishwa na eneo hilo na kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa
kutoa ardhi bure huku akibainisha kuwa ombi kubwa la mwekezaji ni kuwa
na nishati ya kutosha kwa kuwa viwanda hivyo hususani kiwanda cha nguo.
Kwa upande wake
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemhakikishia mwekezaji huyo
upatikanaji wa mahitaji yote muhimu na kuahidi kushirikiana na taasisi
zote za Serikali zinazohusika kuhakikisha anapata huduma zote kwa wakati
na bila urasimu wowote.
Kuhusu suala la
Umeme Mtaka amesema katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 Wizara ya Nishati
kupitia Shirika la umeme TANESCO imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa
kituo cha kupozea umeme(substation) ambacho kitajengwa karibu na eneo la
uwekezaji huo
Mtaka ameongeza
kuwa mtazamo wa mkoa wa Simiyu ni kuwa na viwanda vichache vinavyoajiri
watu wengi badala ya kuwa na viwanda vingi vinavyoajiri watu wachache,
huku akitoa wito kwa wakulima wa pamba kulima pamba kwa wingi kwa kuwa
kiwanda cha nguo kitakuwa mkombozi wa kuongeza thamani ya zao la pamba
na itauzwa kwa bei ya uhakika.
Naye Katibu wa
Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema kujengwa kwa
kiwanda cha nguo mkoani Simiyu kutasaidia wakulima wa pamba kupata soko
la uhakika kuondoa changamoto ya bei ya pamba kwa kuwa kitapanua wigo wa
soko la pamba, ambapo pamba inayotumika hapa ni nchini ni asilimia
20-25 ya pamba yote inayozalishwa.
No comments:
Post a Comment