Sunday, November 17, 2019

SERIKALI KUMSAIDIA MTOTO ANNA

Na Mwandishi Wetu-WAMJW

Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa pole kwa Anna Zambi mwenye umri wa miaka 16, ambaye amefiwa na wazazi wake wote wawili pamoja na ndugu zake watatu.

Waziri Ummy ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo tayari kutoa msaada wa kisaikolojia.

“Pole nyingi kwa binti yetu Anna Zambi, hili jambo ni kubwa mno kwa huyu mtoto, inaumiza sana, ninamwombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,nasi Wizara tukiwa na jukumu na dhamana ya kusimamia ustawi na maendeleo ya watoto nchini tunachukua jukumu la kuratibu na kusimamia psychosocial support ya mtoto huyu pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wake kwa ujumal” alizema Waziri Ummy.

Waziri Ummy alimuagiza Katibu Mkuu Idara  Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu kuratibu masuala ya utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa Mtoto Anna na Katibu Mkuu huyo amemtembela mtoto Anna nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam na kutoa salamu za polekwa niaba ya Wizara.

Akizungumza mara baada ya kutoa salamu za pole Dkt. John Jingu amesema kuwa Wizara imeshatoa Maafisa wa Ustawi wa Jamii  kuanza kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa Mtoto Anna na kuuhakikisha kuwa Serikali itamsaidia Mtoto huyo ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

Ameongeza kuwa Serikali itakuwa bega kwa bega na familia katika kuhakikisha mirathi inasimamiwa vizuri ili aweze kupata haki zake zote bila kuingiliwa na mtu yoyote kwani ni yupo katika wakati mgumu sana kwa kuondokewa na familia yake yote.

“Nikuhakikishie tutasimamia na utapata msaada mzuri na tunaamini utakaa sawa na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuoe nguvu na faraja katika kipindi hiki kugumu unachopitia tuko pamoja na wewe” alisema Dkt. Jingu

Wazazi wa Anna- Lingston Zambi na Winfrida Lyimo pamoja na ndugu zake watatu Lulu, Adrew na Grace walifariki Dunia Oktoba 26 mwaka huu wakiwa njiani kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Kilimanjaro, kwenye mahafali ya Kidato cha Nne ya Anna, ambapo gari waliokua wakisafiria lilisombwa na maji na mafuriko yaliyotokea wilayani Handeni mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment