Sunday, November 17, 2019

Vijana Nchini Wamehimizwa Kushiriki Kuchagua Viongozi wa Serikali za Mitaa


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akiongea na wananchi wa na wanamichezo waliohudhuria kushuhudia fainali ya Kamsese jimbo Cup kati ya timu ya Kikilo dhidi ya Masange mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kisese Disa wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma.
Mbunge wa Kondoa, halmashauri ya wilaya ya Kondoa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akiwasalimia wananchi na kumkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza kuhutubia hadhara na kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya Kamsese jimbo Cup yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kisese Disa wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akipiga
penati kuashiria kuanza kwa mchezo wa fainali ya Kamsese jimbo Cup iliyozikutanisha timu za Kikilo dhidi ya Masange mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kisese Disa wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma ambapo Kikilo iliibuka mshindi kwa kuifunga
Masange 2:1.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akikagua
timu ya Masange kabla ya kuanza kwa mtanange wa fainali ya Kamsese jimbo Cup iliyozikutanisha timu za Kikilo dhidi ya Masange mwishoni mwa wiki katika viwanja vya
Kisese Disa wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (wa tatu
kushoto) akiwasili viwanja vya viwanja vya Kisese Disa wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki kufunga mashindano ya Kamsese jimbo kwa fainali iliyozikutanisha timu za Kikilo dhidi ya Masange. Na wa pili kushoto ni Mbunge wa Kondoa, halmashauri ya wilaya ya Kondoa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Ashatu Kijaji.
Mashabiki wa timu ya Kikilo wakishangilia ushindi wa timu yao mara baada ya
mchezo uliyozikutanisha timu za Kikilo dhidi ya Masange kumalizika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kisese Disa wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma.
(Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM, Kondoa)

********************************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Kondoa
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amewataka vijana kote nchini kushiriki kikamilifu katika kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa ifikapo Novemba 24, mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza wakati akifunga mashindano ya jimbo Cup yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kisese Disa wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma.
Lengo mashindano hayo ni kuhamasisha vijana na wananchi wote kote nchini kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuwa chachu ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo nchini kwa vijana wa umri mbalimbali.
Naibu Waziri amewataka wadau wa michezo kuyatazama mashindano yanayofanyika nchini kuwa ni mkakati wa kuibua vipaji vya vijana katika michezo mbalimbali hatua inakayopelekea kuwa na timu bora za ligi na hatimaye timu za taifa.
“Wito wangu kwa vijana kote nchini, tumieni mashindano ya aina hii kujitokeza na kushiriki kikamilifu ili kuonesha vipaji vyenu, Serikali tumeendelea kuwekeza nguvu kubwa kwenye kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.” amesema Naibu Waziri wa Shonza.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Naibu Waziri Shonza amesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa timu za vijana kwa taifa ambapo alithibitisha kuwa sote tu mashahidi kwa namna ambavyo timu zetu za Taifa za vijana zinavyofanya vizuri katika mashindano mbalimbali na kutoa taifa kimasomaso na kusisitiza tuko vizuri.
Miongoni mwa mashindano ambayo Tanzania imefanya vizuri ni pamoja na mashindano
ya timu kutoka kanda za Afrika Mashariki na Kati ambapo imekuwa washindi wa
mwaka 2019 kwa vijana chini ya miaka 20 (CECAFA U-20), Washindi wa kombe la
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kusini mwa Afrika (COSAFA) kwa timu ya
wanawake ya Tanzanite kwa vijana chini ya miaka 20 (U20-2019), Novemba 15, 2019 timu ya Taifa Stars imewalaza timu ya Equatorial Guinea kwa kuifunga magoli 2-1 kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu Afcon 2021, na October 18, 2019 Taifa Stars ilifuzu kucheza fainali za CHAN zinazotarajiwa kufanyika mwaka 2020 nchini Cameroon.
Mashindano hayo yalishirikisha kata zote 21 za wilaya ya Kondoa yakiongozwa na kauli mbiu ya “Uchaguzi wa Serikali za mitaa ndio msingi wa maendeleo yetu, twendeni tukashiriki pamoja” ambayo inawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo ili kupata viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano kuanzia 2019 hadi 2024.
Aidha, Naibu Waziri Shonza amesema Mbunge na Naibu Waziri wa Fedha Dkt. Ashatu Kijaji ameounga mkono Serikali ya Awamu ya Tano ambapo Sera ya Taifa ya Michezo ya mwaka 1995 inasema jukumu la kukuza na kuendeleza michezo nchini si la Serikali peke yake, bali ni jukumu la Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali akiwemo Mbunge wa Kondoa ambaye amewapa vijana wa jimbo hilo kounesha uwezo na vipaji vyao katika michezo.
Zaidi ya hayo, Naibu Waziri Shonza amesema kuwa mashindano hayo ya Kamsese wilaya ya Kondoa ni chachu ya kupata vijana wanaoweza kucheza timu ya mkoa wa Dodoma, Dodoma FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza na kuwaomba waandaaji wa mashindano hayo pamoja na wadau wengine kutanua na kuongeza wigo wa mashindano hayo yashirikishe pia michezo mingine ikiwemo mpira wa pete, riadhaa, mpira wa kikapu na michezo mingine ili kupata vipaji katika hiyo.
Mkoa wa Dodoma hususani wilaya ya Kondoa kwa historia ya michezo imekuwa ni eneo muhimu linalotoa wanamichezo bora akiwapo mwanariadha mkongwe Mzee wetu Juma Ikangaa ambao ni mfano wa kuiga na ni fursa kwa vijana nchini kuonesha vipaji vyao kwa maendeleo ya taifa lao.
Kwa upande wake Mbunge wa Kondoa, halmashauri ya wilaya ya Kondoa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amezipongeza timu zote za kata za wilaya ya Kondoa kushiriki mashindano hayo kwa amani, upendo na mshikamano na hatimaye kufikia kilele cha mashindano hayo kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Dkt. Ashatu ameeleza kuwa dhamira ya mashindano hayo ni kuileza Tanzania, dunia na kuimbia Kondoa kuwa kuna amani na usalama wa kutosha hatua inayotupelekea kwenda kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na usalama.
“Michezo ni ushirikiano, mshirikamano na kudumisha michezo kwa sababu tunatambua kuwa michezo ni afya, michezo ni ajira na michezo ni furaha tumeungana kwa pamoja” Dkt. Ashatu.
Mashindano ya ligi ya Kamsese yalishirikisha timu kutoka kata 21 za wilaya ya Kondoa ambapo timu zilizofikia hatua ya fainali ni kata za Kikilo na Masange na hatimaye timu ya Kikilo kuifunga Masange 2:1 na kuzawadiwa kombe pamoja na fedha taslimu Sh. 500,000/= na kuandika historia ya kuwa mabingwa wa kwanza wa kihistoria wa mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment