Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen
Nicodemus Mwangela akiangalia paa lililo ezuliwa na mvua ya upepo mkali
katika makazi ya wananchi Wilayani Momba, zaidi ya nyumba 200 wilayani
humo zimeharibiwa.
Nyumba ya mwananchi ikiwa
imebomoka na kuezuliwa kutokana na mvua ya upepo Mkali iliyonyesha jana
jioni na kusababisha uharibifu wa nyumba Zaidi ya 360 katika halmashauri
za Momba na Mbozi Mkoani Songwe.
…………………………
Mvua iliyoambatana na upepo mkali
iliyonyesha jana jioni Mkoani Songwe imesababisha uharibifu wa nyumba
Zaidi ya 360 Katika Wilaya za Mbozi na Momba pamoja na kujeruhi watoto
wawili.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen
Nicodemus Mwangela mapema leo ametoa taarifa hiyo mara baada ya kukagua
hali ya uharibifu wa makazi ya watu na taasisi za serikali ambapo
ameziagiza halmashauri husika kurejesha miundombinu ya serikali
iliyoharibika.
“Kuna wananchi wamepata madhara
lakini wametibiwa na kurejea nyumbani, nawapongeza sana viongozi na
majirani ambao waliwahi kutoa msaada kwa wahanga aidha ninaagiza
halmashauri za Momba na Mbozi warekebishe haraka nyumba za walimu na
madarasa ili huduma ziendelee.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Aidha ametoa pole kwa wahanga na
amewapongeza majirani wa waliopata uharibifu wa nyumba kwa kuwahifadhi
wenzao jana usiku huku akiwa hakikishia kuwa Kamati za Usalama za Wilaya
na wataalamu wanafanya tathmini ya uharibifu na kupanga namna ya kutoa
msaada.
Brig. Jen. Mwangela amewataka
wananchi wote kuchukua tahadhari kwakuwa mvua za Mkoani Songwe ni nyingi
hivyo waimarishe makazi yao pia watoe taarifa mapema endapo utatokea
uharibifu wowote.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi
Hanji Godigodi amesema wataalamu wa Halmashauri wanaendelea na tathmini
ya hali ya uharibifu na kuwa nyumba za walimu na shule zitafanyiwa
marekebisho haraka.
Afisa Mtendaji kata ya Msangano
Halmashauri ya Wilaya ya Momba Focus Kadule amesema baada ya tathmini ya
hali ya uharibifu katika kata yake ataitisha Mkutano wa hadhara ili
wananchi waweze kujitolea kuwasaidia waliopata uharibifu kutokana na
mvua hizo.
Fadeli Ng’aala mkazi wa Kijiji cha
Hamwelo Halmashauri ya Mbozi amesema mvua iliyoambatana na upepo
imeezua paa la nyumba yake huku yeye na watoto wakiwa ndani na
kusababisha uharibifu wa vyakula na vifaa vingine kama vitanda,
magodoro, televisheni, solar na masofa.
Naye Mwalimu Jacob Sambilila wa
Shule ya Msingi Nkala Halmashauri ya Wilaya ya Momba amesema mvua
zilianza saa tisa mchana na kusababisha mti kuangukia darasa hali
iliyozua taharuki kwa wanafunzi lakini pia baada ya kurudi nyumbani
kwake alikuta nyumba anayoishi imeezuliwa.
“Baada ya kutoka kazini nilikuta
nyumba ya mwalimu mwenzangu imeezuliwa na nilipofika kwangu nimekuta
nyumba imebomoka na kuezuliwa na kusababisha uharibifu hata kwenye
chakula chote nilichotunza kimeharibika na vifaa vya ndani.”, amesema
Mwalimu Sambilila.
No comments:
Post a Comment