KAMISHNA WA UHIFADHI AZUNGUMZIA MAFANIKIO KATIKA KIPINDI CHA RAIS MAGUFULI .
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la
Hifadhi za Taifa (TANAPA),Dkt Allan Kijazi akizungumzia mafanikio ya
Shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano
chini ya Mh,Rais Dkt John Pombe Magufuli.
...................
Chini ya uongozi wa awamu ya tano, TANAPA imeweza kufanya mabadiliko makubwa katika eneo la mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa Kiraia kwenda Jeshi-Usu. Muundo mpya wa Shirika uliidhinishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Novemba, 2018.
Hadi kufikia leo jumla ya watumishi 1,919 ambao ni asilimia 86 ya watumishi 2,230 ambao ni kuanzia ngazi ya Kamishna wa Uhifadhi hadi Askari wa Uhifadhi wa kada mbalimbali, wamepatiwa mafunzo ya mabadiliko ya mfumo.
Ongezeko la Hifadhi mpya za Taifa
Tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hifadhi za Taifa mwaka 1959 hadi mwezi Oktoba 2016, Shirika lilikuwa likisimamia hifadhi 16 nchini. Katika kipindi cha Miaka Minne ya Awamu ya Tano, Hifadhi za Taifa nyingine sita (3) za Burigi – Chato; Ibanda – Kyerwa; Rumanyika – Karagwe.
Aidha, hatua mbali mbali zinaendelea za kuyafanya yaliyokuwa Mapori ya Akiba ya Selous kupandishwa hadhi na kuongeza hifadhi nyingine mpya za Nyerere; Kigosi na Mto Ugala ambapo kukamilika kwa hatua hizi kutafanya jumla ya Hifadhi za Taifa kufikia 22 ambazo kwa ujumla wake zitakuwa na eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 104,559.1 ambalo ni takribani asilimia 11 ya eneo la nchi yetu ya Tanzania.
Aidha, TANAPA imeshaanza utekelezaji wa usimamizi wa majukumu katika hifadhi hizi mpya ambayo inalenga kupanua wigo wa utalii wa ukanda wa Kaskazini Magharibi ambao utaunganisha hifadhi hizi na Hifadhi za Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ongezeko la Mapato
Katika kipindi cha Awamu ya Tano, TANAPA imeweza kuongeza mapato ikilinganishwa na makadirio yaliyokuwa yakiwekwa kila mwaka. Shirika limeweza kuongeza mapato kutoka kiasi cha shilingi 175,089,696,000 kilichokusanywa mwaka wa fedha 2015/16; shilingi 207,587,218,000 zilikusanywa mwaka 2016/17 na shilingi 254,794,242,000 mwaka 2017/18 hadi kufikia kiasi cha shilingi 279,406,200,806 mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni ongezeko la shilingi 566,697,964,806 kwa miaka mitatu sawa na asilimia 60.
Ongezeko la mapato ya shirika limetokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa ndani na nje ya nchi ili kuyafikia masoko mapya ambapo liliwezesha kuwa na ongezeko la watalii kutoka wageni 957,576 mwaka 2015/16 hadi 1,141,462 mwaka 2018/19 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.2
Mchango wa Kodi Serikalini
TANAPA imeongeza mchango wa kodi kwa serikali kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2016/2017 hadi kufikia shilingi bilioni 42 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Katika kipindi hiki cha miaka minne ya uongozi wa awamu ya tano, TANAPA imeweza kutenga fedha kiasi cha shilingi 111,374,526,023.00 ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019. Miradi hii imehusisha uimarishaji wa huduma za utalii ikiwemo ujenzi wa maeneo ya malazi ya gharama nafuu (mabanda na hosteli), miradi ya kuongeza bidhaa za utalii, nyumba za wafanyakazi, vifaa vya kazi kama boti, magari na ndege.
Utatuzi wa Migogoro ya Mipaka na Wananchi
Shirika la Hifadhi za Taifa limeweza kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini baina ya hifadhi na wananchi wanaozunguka hifadhi.
Mwaka 2018/2019 Shirika kupitia Mpango wake wa Ujirani Mwema unaoshirikisha jamii katika uhifadhi, liliamua kushirikiana na vijiji vilivyo pembezoni mwa Hifadhi za Taifa kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi pamoja na kuweka alama za kudumu za mipaka kwenye mipaka yote ya Hifadhi.
Kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kumekuwa na jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto za migogoro ya ardhi ikiwemo mipaka na uingizaji mifugo kwa ajili ya malisho.
Kutokana na jitihada hizo, Shirika linagharamia kazi ya kuandaa na kuwezesha mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya vijiji vinavyozunguka Hifadhi za Taifa Tanzania kwa kutumia utaalamu wa tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ‘National Land Use Planning Commission - NLUPC’ yenye mamlaka kisheria. Lengo kuu likiwa ni kuviwezesha vijiji 392 vilivyokuwa vimeainishwa kutokuwa kuwa na mipango hiyo. Hata idadi hii itaongezeka kwa sababu ya Hifadhi mpya ambazo zimeanzishwa.
Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa kazi hii ilianza mwaka wa fedha 2018/2019 kwa kuvilenga vijiji 95 ambavyo kutokana na baadhi ya vitongoji kuwa vijiji, idadi iliongezeka kufikia vijiji 107 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire.
Aidha, kwa kipindi hiki cha miaka minne Serikali kupitia Shirika la TANAPA imetekeleza miradi katika vijiji 101 vinavyopaka Hifadhi za Taifa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa (76), nyumba za walimu (19), mabweni (7), visima vya maji (10), maabara (5), zahanati (10), mabwalo ya chakula (4), lambo la maji (1), madawati (2,175), majengo ya utawala / ofisi ya walimu (10), nyumba za waganga (16), mizinga ya nyuki (1,497), nyumba kwa ajili ya kuzalisha uyoga (1), miradi ya ufugaji wa samaki (2), kuanzisha Benki za Uhifadhi za kijamii (21), kutoa taa za umeme-jua kwa ajili ya vikundi vya uvuvi (80), boti kwa ajili ya vikundi vya uvuvi (2), Injini za boti kwa ajili ya vikundi vya uvuvi (2).
Vita Dhidi ya Ujangili na Ongezeko la Idadi ya Wanyama walio hatarini kutoweka
TANAPA imeweza kuimarisha mifumo ya ulinzi wa wanyamapori na ustawi wa wanyama adimu na kupelekea ongezeko la wanyama adimu jamii ya faru kwa asilimia 10 katika Hifadhi za Taifa na kudhibiti vitendo vya ujangili kwa zaidi ya asilimia 90. Aidha Majangili 14,464 wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo mbalimbali ya dola nchini.
Ongezeko la Masoko Mapya ya Watalii na idadi ya vitanda
Kumekuwepo na ongezeko la idadi ya watalii wa nje kutoka 518,457 hadi 715,314 kutokana na kuongezeka kwa wigo wa soko la utalii katika masoko mapya katika Bara la Asia na Mashariki ya Mbali hususani Israeli, Uturuki, China na Urusi.
Aidha, kumekuwepo na ongezeko la vitanda vya watalii kutoka vitanda 2400 hadi kufikia vitanda 5,829 vya watalii wa nje (international tourists), na vitanda 3,601 hadi kufikia 4,970 vya wageni wa ndani (domestic tourists) na kufanya jumla ya vitanda vyote kufikia 10,799
Utekezaji wa Miradi mbalimbali ya Kimkakati kama vile:
- Ununuzi wa kivuko katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo
- Ujenzi wa hoteli ya hadhi ya nyota tatu katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo
- Ujenzi wa uwanja wa mpira wa golfu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti
- Ununuzi wa boti ya kifahari ya kitalii katika hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane
- Ujenzi wa eneo maalumu la kuhifadhi wanyama aina ya faru kwa ajili ya shughuli za kitalii katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi.
Kuongezeka kwa huduma za utalii kama vile:
- Utalii wa Puto (Baloon safaris)
- Uendeshaji wa farasi (Horse riding)
- Upandaji Mlima Kilimanjaro kwa kutumia baiskeli (mountain cycling)
- Kuruka na mwavuli (paragliding)
- Kuhamisha na kupandikiza wanyama katika hifadhi mbalimbali
No comments:
Post a Comment