Sunday, November 17, 2019

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU WAZIRI WA KILIMO KUBAINI UBADHIRIFU WA BILIONI 53.2 BODI YA KOROSHO TANZANIA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari Ofisi ndogo ya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma kuhusu ubadhilifu alioubaini kwenye malipo ya wakulima wa korosho. Wengine pichani ni Naibu Mawaziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Kulia) na Mhe Hussein Bashe (Kushoto) (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari Ofisi ndogo ya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma kuhusu ubadhilifu alioubaini kwenye malipo ya wakulima wa korosho.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari Ofisi ndogo ya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma kuhusu ubadhilifu alioubaini kwenye malipo ya wakulima wa korosho.

Dodoma, 17 Novemba, 2019

Ndugu Wanahabari;
Kama mnavyofahamu, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitoa maelekezo ya kuwa katika msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019 kuwa Serikali itanunua korosho zote za Wakulima ili kuwaondoa kwenye kusuasua kwa bei ya korosho.

Tarehe 12/11/2018 Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Korosho Tanzania ilianza kutekeleza agizo la Mhe. Rais kwa kuunda Kamati Maalum ya kusimamia zoezi la ununuzi wa korosho ghafi kutoka kwa Wakulima wa mikoa ya Pwani, Lindi Mtwara na Ruvuma.

Jumla ya korosho zote zilizokusanywa zilikuwa ni tani 222,561.1 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 732.8.  Korosho hizo zilikuwa za madaraja mawili ambayo ni daraja la kwanza (Standard grade) tani 204,476.1 zenye thamani ya Shilingi 674,522.700 na daraja la pili (Under grade) tani 18,084.9 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 47,744,294,400.  Hadi sasa Serikali tayari imelipa kwa wakulima jumla ya Shilingi Bilioni 707.8 sawa na tania 217,786 za korosho ghafi.
Aidha,hivi karibu Mhe.Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Fedha kutoa Shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kuwalipa wakulima na watoa huduma wengine waliokuwa wanadai malipo yao ya korosho msimu wa 2018/2019.

Ndugu Wanahabari;
Nimewaita ili niwafahamishe kwa nini hadi leo hatujakamilisha zoezi la kuwalipa wakulima hao kutokana na sababu kadhaa:
Kwanza; imeonekana kuwa kuna udanganyifu mkubwa ambao umefanywa na Viongozi wa Vyama vya Msindi katika mkoa wa Pwani. Mfano Chama cha Msingi cha (Sanga Sanga AMCOS) katika msimu uliopita; walikusanya kilo 212 tu lakini kwenye hesabu imeonekana walifanya udanganyifu na kuongeza kilo elfu saba zaidi (7,000).  Aidha, walitoa taarifa ya uongo kuhusu uwepo wa korosho za daraja la kwanza za kilo 244 badala ya daraja la pili, udanganyifu huo, ulisababisha Serikali kulipa zaidi ya shilingi Milioni 222,328,867 kwenye Chama hicho cha Msingi (Sanga Sanga AMCOS).

Mfano mwingine, katika mkoani Mtwara, wilaya ya Tandahimba.  Timu ya Uhakiki ya Wizara iligundua malipo hewa ya Shilingi Bilioni 1.6.  Wizara ya Kilimo tumepata wasiwasi na kutilia shaka mwenendo wa uadilifu wa baadhi ya Viongozi wasio waaminifu.  Tumeamua kuchukua hatua ili tujiridhishe kabla ya kufunga msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka 2018/2019.

Ndugu Wanahabari,
Kutokana na mapungufu hayo, nimeamua kuunda Timu ya Uchunguzi ya watu watano (5) ili washirikiane na Timu ya uhakiki ya Wizara ya Kilimo kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa mwenendo mzima wa biashara ya korosho kwa msimu wa 2018/2019.  Timu zote mbili zitafanya kazi kuanzia sasahadi tarehe 15 Januari, 2020.

Pili, Timu ya Uchunguzi; itatakiwa kuhakiki majina ya Wakulima kutoka kwenye Vyama vya Msingi, kwenda Vyama Vikuu na baadae Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwenda kwenye mfumo wa malipo ya Benki ili kubaini fedha walizolipwa Wakulima zililipwa kupitia, akaunti zao.
Tatu, Timu ya Uchunguzi; itatakiwa kuchunguza kama kulikuwa na unyaufu kwenye korosho zote, zilizonunuliwa kwenye msimu wa 2018/2019 na kama unyaufu ulikuwepo, ulikuwa ni wa kiwango gani ili Serikali itoe taarifa inayoendana na uhalisia.

Ndugu Wanahabari;
Aidha, mtakumbuka kuwa Desemba, 2016 Serikali iliamua kuufuta Mfuko wa Wakfu wa Maendeleo ya zao la Korosho (Cashewnut Development Trust Fund - CDTF) na baadae majukumu yake, yalikasimiwa na Bodi ya Korosho, wakati Mfuko huo unafutwa ulikuwa na fedha taslimu Benki shilingi Bilioni 53.2.  Fedha hizo kazi yake ilikuwa kuendeleza tasnia ya korosho ambapo jukumu kubwa lilikuwa ni kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho na ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho.  Viwanda hivyo vilikuwa vijengwe eneo la Mkinga (Tanga), Mkuranga (Pwani) na Tunduru (Ruvuma).

Jambo la kusikitisha ni kuwa, Bodi ya Korosho ilishindwa kutekeleza majukumu hayo ya kujenga viwanda hivyo na ghala badala yake fedha hizo zilitumika kinyume na makusudio. Jambo baya zaidi kuna viashiria ambavyo vinatia shaka na kutoa tahadhari ya kufanyika kwa haraka kwa uchunguzi wa kina wa namna fedha hizo zilivyotumika. Viashiria hivyo ni pamoja na matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 600 zilizotumika kwa ajili ya kulipia gharama za uandaaji wa mikutano ya Wadau, pamoja na malipo ya pembejeo kiasi cha zaidi ya Bilioni 28 na malipo kwa Watoa huduma (Wauzaji wa magunia). Malipo ya shilingi Bilioni 12 ambayo yameonekana, yalishalipwa kwa watoa huduma hao.

Malipo mengine tunayotilia mashaka ni pamoja na Bodi ya Korosho kuvilipa Vyama Vikuu vya TANECU Bilioni 1.8, CORECU Bilioni 2.1 kwa maelezo kuwa hayo ni madai ya miaka iliyopita ambapo Bodi ya Korosho ilikuwa ikidaiwa.

Ndugu Wanahabari;
Nimalizie kwa kusema, baada ya kuona kuna viashiria na mwenendo usioridhisha, naelekeza kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uhakiki na uchunguzi ili kuangalia namna kiasi cha fedha cha shilingi Bilioni 53.2 zilivyotumika na kama itabainika, wale wole waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo za umma wachukuliwe hatua kwa mujibu ya sheria za nchi.

Japhet Hasunga (Mb)
WAZIRI WA KILIMO

No comments:

Post a Comment