Wednesday, November 20, 2019

MAKUSANYO KODI YA ARDHI GAIRO HAYAMFURAHISHI NAIBU WAZIRI MABULA


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia wamiliki wa viwanja walioingizwa katika Mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya Kieletroniki katika ofisi za Ardhi za Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya hiyo jana. Wa tatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe na aliyekaa ni Afisa Ardhi Msaidizi wa Halamashauri ya Wilaya ya Gairo Salivius Sarapion.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Gairo Agnes Mkandya kuhusiana na makusanyo ya kodi ya ardhi wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro jana. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe akiangalia sehemu ya Mizinga ya Nyuki katika eneo la Msingisi Gairo wakati wa ziara yake katika wilaya ya Gairo jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akielekea katika Shamba la Miti la Ukaguru kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe na Kulia ni Meneja wa Shamba la Miti la Ukaguru Mohamed Msalu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka kukagua ujenzi wa ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana katika hifadhi ya Msitu wa Ukaguru. Anayemfuatia ni Mkuu wa wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo wakitembea katika hifadhi ya Msitu wa Ukaguru wilaya ya Gairo jana alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Gairo kwenye Maporomoko ya hifadhi ya Msitu wa Ukaguru wilayani Gairo jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Gairi Sirieli Mchembe.
……………………

Na Munir Shemweta, WANMM GAIRO

Kasi ndogo ya ukusanyaji mapato ya Kodi ya pango la ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro imemsononesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ta Makazi Dkt Angeline Mabula na kuagiza halmashauri hiyo kuongeza kasi ili kufikia lengo la mapato ya kodi ya ardhi.

Akiwa katika ziara yake ya siku moja katika wilaya hiyo jana tarehe 19 Novemba 2019 Dkt Mabula alielezwa na Afisa Ardhi katika halmashauri ya Gairo Nicolaus Matsuva kuwa halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka 2018/2019 imekusanya  shilingi milioni 12.3 na mwaka huu kufikia Novemba imekusanya milioni 10 ya kiwango ilichopangiwa cha milioni 55.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kiwango hicho cha makusanyo katika halmashauri ya Gairo ni kidogo na hakijafikia hata nusu ya makadirio ya shilingi milioni 55 iliyowekewa halmashauri hiyo kukusanya kwa mwaka na makadirio hayo hayalingani na uhalisia wa makusanyo ya halmashauri.

Aliitaka halmashauri ya Gairo kupitia idara yake ya ardhi kuongeza kasi ya makusanyo ya maduhuli ya kodi ya pango la ardhi kwa kuwa kodi hiyo ndiyo inayoisaidia serikali  kutekeleza miradi mikubwa aliyoieleza kuwa mingi inataegemea kodi ya ndani.


‘’Msipokusanya kodi ya ardhi mjue mnamkwamisha Mhe Rais kutekeza miradi mikubwa kama vile mradi wa kufufua umeme wa Mwl. Nyerere maarufu  kama stiglers hivyo ni lazima tuongeze kasi ya makusanyao’’ alisema Dkt Mabula.


Sambamba na hilo Dkt Mabula aliitaka halmashauri ya wilaya ya Gairo kuhakikisha kufikia Desemba 2019 inarejesha fedha shilingi milioni 31 ilizopatiwa mwezi Juni 2019 kama mkopo kwa ajili ya upimaji viwanja katika halmashauri hiyo.


Hatua hiyo inafuatiwa Naibu Waziri Mabula kuhoji kuhusiana na marejesho ya fedha za mkopo huo na kuelezwa na Afisa Ardhi kuwa, halmashauri hiyo hajarejesha kiasi chochote cha fedha za mkopo iliopatiwa kwa ajili ya upimaji viwanja na kuomba kuongezewa muda wa kurejesha hadi mwezi Machi 2019.


‘’ Toka mwezi Juni hadi leo Desemba hamjarejesha wakati ulitakiwa kurejeshwa ndani ya miezi mitatu, Mkopo huu unazunguka kwa nini hamjarejesha hadi leo? Kazi mliyopewa hamjamaliza naagiza hadi kufikia Desemba fedha hiyo iwe imerejeshwa’’ alisema Mabula.


Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameshangazwa na idara ya ardhi katika halmashauri ya Gairo kuingiza viwanja 155 kati ya 1,198 kwenye mfumo wa makusanyo ya kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki jambo alilolieleza linaikosesha serikali mapato yataokanayo na kodi ya pango la ardhi sambamba na kushindwa kutoa ilani kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ingawa ilani  hizo zilizndaliwa tangu mwezi Machi 2019.


Dkt Mabula alielezwa na Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Gairo Nicolaus Matsuva kuwa, baadhi ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi walishindwa kupatiwa ilani hizo kutokana na maeneo wanayomiliki kukutwa wakiishi watu wengine tofauti na wamiliki waliopo kwenye kumbukumbu zao jambo lilimfanya Naibu Waziri kumuagiza Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda Maalum ya Morogoro Erick Makundi kufuatilia suala hilo kwa kwenda uwandani na kupatiwa taarifa kufikia Desemba mwaka huu.


Kwa upande wake Mkuu  wa Wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe alisema, wilaya yake ina changamoto kubwa ya ujenzi holela na kubainisha kuwa hata zoezi la urasimishaji katika wilaya hiyo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo sebule za baadhi ya nyumba kuelekezwa kwenye vyoo vya nyumba nyingine.


Hata hivyo, alimuahidi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa ikiwemo uandaaji wa Mpango Kabambe katika wilaya hiyo iweze kupangika kimji sambamba na kuwa na Mji wa Serikali utakaojumuisha taasisi zote za serikali zilizopo katika wilaya hiyo.


Ktika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitembelea hifadhi ya Msitu wa Ukaguru uliopo Tarafa ya Nongwe kata ya Mandege wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  unaofanywa na Shirika la nyumba la Taifa (NHC).


Akiwa kwenye ukaguzi wa ujezi huo, Dkt Mabula alipata malalamiko ya baadhi ya vibarua wanaojenga ofisi hiyo kutopatiwa malipo kwa wakati jambo walilolieleza kuwa linawakatisha tamaa kuendelea na kazi hiyo. Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula aliwataka vibarua hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuahidi kulifuatialia suala hilo haraka ili vibarua hao walipwe fedha kwa wakati.


Aidha, Dkt Mabula alipata fursa ya kutembelea Maporomoko katika hifadhi ya shamba la Miti la  Ukaguru ambapo alijionea namna eneo hilo linavyoweza kuwa moja ya vyanzo vya umeme sambamba na kuwa kivutio kikubwa cha utalii kinachoweza kuingizia serikali mapato yatokanayo na sekta hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe alielezea ziara ya Naibu Waziri Mabula kwenye Maromoko hayo kuwa ni ya kwanza kufanywa na Waziri na kubainisha kuwa ziara hiyo inaweza kuwa chachu ya hifadhi ya Msitu huo kutumika kwa shughuli mbalimbali kama vile za kitalii.

No comments:

Post a Comment