Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh.
Justin Malisawa (kaunda suti ya bluu) akifurahi pamoja na washiriki wa
kongamao la wanawake wajasiliamali kuwezeshwa kiuchumi katika ukumbi wa
Manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya Wanawake wajasiliamali
waliohudhuria katika kongamano lililolenga kutoa mafunzo ya kurasimisha
shughuli zao paoja na kutambua fursa mbalimbali za kujipatia kipato
zilizopo katika maeneo yanayowazunguka katika mji wa Sumbawanga.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa
…………………..
Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Sumbwanga Mh. Justin Malisawa amewataka wanawake mkoani Rukwa kuachana
na dhana kuwa familia zinazopendelea kula mboga za majani ni masikini
na hivyo kupelekea kinamama wengi kushindwa kula mboga za majani
kuhofia kuitwa masikini jambo linalopelekea udumavu kuendelea kuwepo
kaika mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa udumavu unatokana na
wananchi wa Mkoa wa Rukwa kula mlo wa aina moja pamoja na kuwa ni
miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji nchini na
kusisitiza kuwa mboga za majani ni muhimu kwa wanawake hasa wajawazito
kwani huwasaidia kuwajenga na kumjenga kiumbe aliyemo tumboni mwake
kukua kiafya na kiakili.
“Na bahati mbaya tumejijengea
utaratibu kwamba familia ambayo inayokula mboga za majani kwa wingi ni
familia masikini, huo ndio ukweli ukimkuta mama Fulani kakarangiza mboga
za majani, kesho mboga za majani, keshokutwa mboga za majani, majirani
watamwita masikini wa kutupwa,” Alisema.
Mstahiki Meya ameyasema hayo
kwenye kongamano la wanawake wajasiriamali lililofanyika katika ukumbi
wa mikutano wa manispaa ya Sumbawanga, kongamano ambalo lilihudhuriwa na
viongozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo mabenki, bima ya
afya, SIDO, TRA, TBS na watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii kutoka
ofisi ya mkurugenzi wa manispaa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa Manispaa ya Sumbawanga George Lupilya amesema kuwa Manispaa
Sumbawanga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imejipanga kuhakikisha
inatekeleza maagizo na Sera mbalimbali za nchi ili kuhakikisha
Mwananchi anafikiwa kwa huduma za Kijamii na kujikwamua Kiuchumi.
Aidha, Kaimu huyo ambaye pia
ni Mkuu wa Idara ya Kilimo amewaasa kinamama hao kuhakikisha
wanajishughulisha na kilimo cha bustani za mboga mboga kwa kulima walau
tuta moja ama mawili ili kuweza kupambana na udumavu pamoja na utapiamlo
katika mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara
ya Maendeleo ya jamii Manispaa ya Sumbawanga Frank Mateni amesema kuwa
dhumuni la kufanya kongamano hilo ni kuamsha ari, kuwajengea uwezo
wanawake wajasiliamali kuona ni fursa gani ambazo wanazo katika
mazingira yao wanayoishi wanayoweza kuyatumia kujiongezea kipato.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na
wanawake wajasilimali zaidi ya 570 wakiongozwa na viongozi wa Jukwaa la
Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Rukwa.
No comments:
Post a Comment