Waziri wa Sayansi na Tekinolojia,
Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza katika Kituo cha kulelea wazee cha
Nunge, kilichopo katika kata ya Vijibweni, wilayani Kigamboni, jijini
Dar es Salaam, kabla ya kutoa msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali
kwa wazee waliyopo kituoni hapo, Novemba 15, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
………………..
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema jamii inatakiwa kuwajali na
kuwatunza wazee na watu wenye mahitaji maalumu kwani hilo ni jukumu la
watu wote na si kuiachia Serikali pekee.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa,
Novemba 15, 2019) wakati wa kikundi cha wake wa viongozi nchini cha New
Millenium Group kilipotembelea makazi ya wazee ya Nunge katika kata ya
Vijibweni Wilaya ya Kigamboni jijini, Dar es Salaam na kutoa misaada wa
vitu mbalimbali.
Waziri Ndalichako amesema kuwa
‘’jukumu la kutunza wazee ni letu sote, nawashukuru wake wa viongozi kwa
umoja wenu, nawaomba muendelee na moyo huu wa kuwasaidia watu wenye
mahitaji maalumu.”
Amesema Serikali imefanya
ukarabati wa nyumba 10 kati ya 50 zilizopo katika makazi hayo ya wazee
na itaendelea kuzikarabati nyumba zote zilizobaki na kujenga uzio ili
makazi hayo yasiingiliwe na watu wanaozunguka eneo hilo.
Naye,Mwenyekiti wa New Millenium
Group, Mke wa Waziri Mkuu Msaafu, Mama Tunu Pinda amesema akinamama hao
wamekesha usiku na mchana kuhakikisha wazee hao wanapata mahitaji na
wametoa walichobarikiwa na Mwenyezi Mungu.
‘’Kikundi chetu katika kutimiza
miaka 10 tangu kianzishwe tumeamua kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutoa
tulichobarikiwa. Ikumbukwe kuwa nasi ni wazee watarajiwa ni asilimia
nne tu ya wazee wanapata mafao wengine hawana msaada wowote. Wazee
kuanzia miaka 60 hunyemelewa na magonjwa mbalimbali hivyo jamii
isiwasahau.”
Kwa upande wake, Mlezi wa kikundi
hicho, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewashukuru akinamama
wenzake wanaounda umoja huo na kuiomba jamii iwaunge mkono.
“Akina Mama wa Millennium mmekuwa
mfano bora kwa wenzetu nawaomba tudumishe umoja wetu na tunamshukuru
Mama yetu Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli kwa kuungana nasi katika
kuwapa tabasamu wazee wetu wa Nunge.”
Awali, Afisa Mfawidhi wa kituo
hicho Jacklina Kanyamweri amewashukuru akinamama kikundi cha New
Mellinium Group kwa kuwakumbuka wazee na watu wenye uhitaji ambapo
amewaomba wasichoke kwani wazee wana mahitaji mengi ikiwemo ujenzi wa
uzio katika makazi hayo na ukarabati wa barabara.
Akina Mama wanaounda umoja huo
wametoa misaada wa vitu mbalimbali ikiwemo sabuni, nguo, gypsum,
baiskeli za watoto, mafuta. Wametembelea kituo hicho wakiwa katika
maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa umoja huo.
Kadhalika, akinamama hao wameahidi
kukarabati bwalo la wazee hao na kujenga mnara wa tenki la kuhifadhia
maji pamoja na kutengeneza mfumo wa maji unaopeleka katika nyumba za
wazee hao kadri Mwenyezi Mungu atakavyowajaalia.
Kwa upande wao, wazee wanaotunzwa
katika makazi hayo wameiomba Serikali kutowatupa na wamewashukuru
akinamama wa New Millennium Group kwa moyo wao wa pekee kwa
walivyojitoa.
No comments:
Post a Comment