Mkurugenzi Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati,
Raphael Nombo,(kulia)akibadilishana jambo na viongozi wengine mara
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela(katikati) kufungua
kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake
kilichofanyika mkoani humo.kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa
TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela ( watatu kushoto waliokaa) akiwa
katika Picha ya pamoja ya washiriki wa Kikao kazi cha
Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara
ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani humo.
Sehemu ya Sekretarieti ya kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa
Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi
zilizochini yake kilichofanyika mkoani tanga, kutoka wizara ya nishati,
kutoka kushoto ni Zaituni Nkya( katikati), Lilian Lumbila na Talkisia Eriyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela (katikati)akizungumza wakati
akifungua Kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na
Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini
yake kilichofanyika mkoani humo.
Mkuregenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Dkt.Tito
Mwinuka( katikati) akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha
Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa
Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
************************************
Na Zuena Msuya, Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amewataka watumishi wa Umma
kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi, Uadilifu, utiifu, weledi,
taratibu na sheria za kazi katika kutumiza majukumu yao kila siku.
Shigela alisema hayo, Novemba 14, 2019 kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi
ya Rais, Utumishi, Dkt. Laurian Ndumbaro, wakati akifungua Kikao kazi cha
Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu wa
Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Shigela aliwaeleza washiriki wa mkutano
huo kuwa pia wanatakiwa kufanya kazi kwa kutumia Lugha safi na sahihi
kulingana na huduma wanayoitoa kwa mtumishi au mteja katika eneo
husika.
Alisema endapo Wakurugenzi na Mameneja wa Rasilimaliwatu watafanya
kazi zao kwa misingi inayotakiwa, hakika kazi zote na miradi mbalimbali
inayotekelezwa na serikali itafanyika kwa umakini mkubwa na kukamilika
kwa wakati.
Vilevile itasaidia wao pamoja na watumishi na wafanyakazi waliochini yao
kujilinda na kuwaepusha na vishawishi dhidi ya rushwa katika sehemu zao
za kazi.
Alifafanua kuwa Wakurugenzi na Mameneja ndiyo wenye dhamana kubwa
ya kusimamia watendaji na watumishi walio chini yao sehemu za kazi,
hivyo wanapaswa kutimiza majukumu kwa weledi ili kuwawezesha
watumishi wanaowaongoza kutekeleza majukumu kwa ufanisi na bila
malalamiko.
Aidha, Shigela aliipongeza Wizara ya Nishati, kwa kuwa wizara ya kwanza
kutekeleza agizo la Katibu Mkuu, ofisi ya Rais, Utumishi lililoelekeza wizara
zote nchini kuweka utaratibu wa kufanya vikao kazi na taasisi zilizochini
yake ili kubaini changamoto na kuboresha mambo mbalimbali katika
Utendaji kazi na usimamizi wa Rasilimaliwatu.
“Watumishi wa umma wanahitaji kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao,
kwa kuwa wao ni kiungo muhimu cha kufinikisha na kuwafikia wananchi
moja kwa moja yale mengi mazuri yanayotekelezwa na serikali kwa
wananchi wake, pia ni watu wanaotumia muda kazini kuliko katika
familia zao, hivyo wasiposimamiwa vizuri na kupata miongozo sahihi ,
yale mazuri
yanayofanywa na serikali hayata wafikia wananchi kama inavyotakiwa”,alisisitiza Shigela.
Akizungumzia suala la kuwaongezea uwezo watendaji na watumishi,
Shigela alizishauri Wizara na Taasisi mbalimbali kuweka utaratibu wa
kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara watumishi wao ili kuendana na
teknolojia inayokuwa kila siku na kuwapa motisha kazini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) Dkt.Tito Mwinuka, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, Dkt.Khamis Mwinyimvua, alisema kuwa utaratibu wa
kufanya vikao na kuzungumza na Tasisi zilizochini ya Wizara imesaidia
sana kuongeza ushirikiano kati ya mtumishi na muajiri.
Pia vimesaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili
wafanyakazi na watumishi ikiwemo kuondoa ama kupunguza malalamiko
kati ya wafanyakazi na waajiri katika maeneo ya kazi.
Vilevile, imeboresha na kuinua ari ya utendaji kazi kwa watumishi na
wafanyakazi wa maeneo husika kwa kuwa haki zao za msingi zinatatuliwa
wakati sahihi.
Sambamba na hilo, Dkt.Mwinuka alisema kuwa imesaidia wafanyakazi na
watumishi wengi kuzungumza na kuweka wazi changamoto zinazowakabili
kwa kuwa zinasikilizwa, na kupatiwa majawabu pamoja na kuelezwa
hatua zinazochukuliwa dhidi ya changamoto hizo kabla ya kutatuliwa.
“Utaratibu huu ni mzuri sana umeleta matokeo chanya, Taasisi na Wizara
tunajua uhitaji na changamoto zinazowakabili wafanyakazi na watumishi
wa sekta zetu kila inapotea, na tunafahamu ni namna gani
tunazishughulikia kwa pamoja na kwa haraka zaidi tofauti na ilivokuwa
huko nyuma, naupongeza sana huu utaratibu” alisema Dkt. Mwinuka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, alimshukuru Mkuu
wa Mkoa huyo na kumuhakikishia kuwa wao kama wasimamizi wa
watumishi na wafanyakazi katika Wizara, Taasisi na Idara mbalimbali za
Serikali watafanya kazi zao kwa uadilifu, weledi,ubunifu na kujituma kwa
kuzingatia misingi na taratibu za kazi.
Alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa, Wizara ya Nishati ni moja ya nguzo
kubwa na muhimili muhimu Sana katika kuchangia maendeleo ya uchumi
kwa kuwezesha kupatikana kwa Nishati ya Umeme nchi nzima, hivyo
wanajukumu kubwa la kuwasimamia vyema watendaji, watumishi na
wafanyakazi ili na wao wafanye kazi zao kwa weledi ,kujituma, ubunifu kwa
maslahi makubwa ya Taifa.
“Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda kila
kona ya nchi yetu, Wizara ya Nishati, sisi ndiyo tunadhamana kubwa
sababu tunazalisha umeme unaotumika katika viwanda hivyo,
tunawahakikishia watanzania kuwa tunatekeleza majukumu yetu usiku na
mchana bila kuchoka kuhakikisha umeme mwingi na wakutosha
unapatikana wakati wote katika maeneo ya uzalishaji hasa viwandani
kutimiza lengo lililokusudiwa,” alisisitiza Nombo.
Nombo alisema kuwa hicho ni kikao cha tatu kufanyika ambapo kikao cha
kwanza kilifanyika Mikoani Dar ES salaam, cha pili mkoani Mwanza,
ambavyo vinafanyika kila robo mwaka, ikiwa ni utaratibu waliojiwekea
katika wizara hiyo na Tasisi zake ili kuzungumza na kujadili mambo kadha
yanayojikeza kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kutatua changamoto
endapo zimejitokeza.
No comments:
Post a Comment