************************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote wahakikishe kuwa
vijana wanawezeshwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Ametoa agizo
hilo leo (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua maadhimisho ya
wiki ya vijana kitaifa mwaka 2019 kwenye viwanja vya Mpilipili, nje
kidogo ya mji wa Lindi.
“Vijana tushirikiane
na Serikali na kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za
Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea
wananchi maendeleo. Hatua hii itatuwezesha kama Taifa tuvuke na tufikie
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema.
Amesema
wakati anatembelea mabanda ya maonesho, ameona ubunifu wa kijana ambaye
ameunda mashine ya kumsaidia mtoto njiti apate joto na pia amemuona
kijana mwingine ambaye amebuni mtambo wa kupukuchua magunia 100 ya
mahindi kwa saa.
Pia
alitembelea banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini,
Argentina, Arzebhaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira
magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonesho hayo ili
kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.
“Nimefurahi
kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa
kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu.”
Akizungumzia
mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya
Waziri Mkuu kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, imeanza kutoa
mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba
(greenhouse) katika mikoa yote na Halmashauri zote nchini.
Amesema
teknolojia hiyo itawasadia wakulima kupata mazao mengi katika eneo dogo
na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya
nchi. “Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika
sekta ya kilimo,” amesema.
Waziri Mkuu
amesema mkakati huo ni utekelezaji wa agizo la Chama cha Mapinduzi
ambacho kinatambua kuwa sekta ya kilimo ndiyo kimbilio la wananchi walio
wengi na kupitia ilani yake ya mwaka 2015 Ibara ya 6 (a) imeielekeza
Serikali “kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa,
pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za
kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao”.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini
zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na
maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.
“Kwa mujibu
wa taarifa tulizonazo, hadi mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya ekari
217,882.36 zilikwishatengwa. Ninaziomba Halmashauri zote zisimamie na
kutekeleza agizo hilo ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumiwa kama
ilivyokusudiwa,” amesema.
Moja ya
shughuli zitakazofanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka
huu ni kuwa na kongamano la vijana linalojumuisha nchi za Afrika Kusini,
Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Uganda na Angola. Miongoni mwa masuala
yatakayojadiliwa ni mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere
katika maendeleo ya Afrika; Mabadiliko katika elimu na ukuzaji ujuzi
kuelekea uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025; na Matumizi ya sayansi,
teknolojia na ubunifu kuelekea uchumi wa viwanda.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi
huo, Waziri wa Nchi OWM – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema sambamba na maboresho ya Sera
ya Elimu na Mafunzo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa
Programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi
mbalimbali za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali.
“Mpaka sasa,
vijana wapatao 32,736 wameshapata mafunzo na mwaka huu, Ofisi ya Waziri
Mkuu vijana wengine 46,000 watapata mafunzo mbalimbali ikiwemo kilimo
cha kisasa,” alisema.
Naye, Waziri
wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Balozi Ally Abeid Karume amewataka vijana kote nchini
washikamane kwenye shughuli zao za uzalishaji mali na pia amewasisitizia
haja ya kuwa wazalendo.
“Vijana
mnategemewa kuwa wazalendo. Kuna tofauti kati ya kuwa raia na kuwa
mzalendo. Uraia unaupata kwa kuzaliwa na uzalendo unaonekana kwa vitendo
na hasa kwa kuwa na maadili mema,” alisema.
“Pia vijana
mnategemewa muendelee kuwa wachapakazi. Naomba msonge mbele zaidi na
mfanye kazi kwa bidii ili muweze kumudu ushindani katika mataifa ambayo
yako mbele kiteknolojia zaidi yetu. Serikali zenu zote mbili zitaendelea
kuunga mkono shughuli za vijana za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa
kimataifa.”
No comments:
Post a Comment