Mkuu wa Wilaya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabagangan Talaba amezindua kampeni ya kutoa elimu kwa kujiepusha na aina zote za vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na vitendo hivyo (MTAKUWWA) kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Uzinduzi wa kampeni hiyo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya Kishapu kwa kushirikiana na Shirika la kueteta haki za wanawake na wasichana KIVULINI ulifanyika Septemba 30, 2019 katika Kata ya Talaga.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Talaba aliwasihi wananchi kujitafakari na kuachana na vitendo vya ukatili katika jamii akisema Serikali haiwezi kuruhu vitendo hivyo kuendelea wakati ambao imedhamiria kuelekea kwenye uchumi wa kati.
"Sisi tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati, hatuwezi kupeleka watu kwenye uchumi wa kati wakiwa na maskitiko, wananyanyasana, hawajitambui, lazima tufike huko tukiwa tunafanana na uchumi wa kati" alisisitiza Talaba.
Aidha Talaba alisema kampeni ya ina hiyo mwaka jana ilihusisha viongozi wa ngazi mbalimbali na kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo baadhi ya viongozi, waalimu na wazazi kutotimiza vyema wajibu wao na hivyo kusababisha maadili kumomonyoka hususani kwa vijana hivyo kampeni ya mwaka huu itakuwa na manufaa zaidi baada ya kuwashirikisha wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema shirika hilo linatekeleza mpango wa MTAKUWWA tangu mwaka 2017 ambapo kwa Mkoa Shinyanga linafanya kazi katika Halmashauri za Kishapu na Shinyanga Vijijini kwa kushirikia na viongozi na wadau mbalimbali kutoa elimu katika jamii.
Alisema baada ya kutoa elimu hiyo, imebainika baadhi ya wazazi wanashiriki vitendo vya kishirikina ikiwemo kuwapaka watoto wao wa kike dawa "samba" ili wawe na mvuto kwa wanaume na kuolewa ili wapate mali jambo ambalo linachochea ongezeko la mimba za utotoni, utoro kwa wanafunzi na hivyo baadhi yao kufukuzwa shule.
Na George Binagi
Vikundi vya ulinzi wa jamii (Sungusungu) vikiwasili kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo kwa kucheza ngoma za asili ya kabila la kisukuma.
Wananchi na Sungusungu wakiwasili kwenye kampeni hiyo kwa njia ya maandamano ya amani.
Wanafunzi kutoka Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari wakiwasili kwenye kampeni hiyo.
Akina mama wilayani Kishapu wakiwasili kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mkuu wa Wilaya Kishapu, Nyabagangan Talaba (kushoto) akicheza pamoja na kikundi cha ulinzi wa jamii kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mkuu wa Wilaya Kishapu, Nyabagangan Talaba akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akitoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi.
Wanafunzi kutoka Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari wilayani Kishapu wakiwa kwenye uzinduzi huo.
No comments:
Post a Comment