Baadhi ya Wanachama wa vyama
Mbalimbali vya Ushirika Mkoani Rukwa wakisikiliza Nasaha za Mkuu wa mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) katika Mkutano
Ulioitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kuwaunganisha wakulima
pamoja kupitia chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo,akizungumza na wananchama wa vyama vya ushirika
………………….
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amevitaka vyama vya ushirika katika Mkoa wa Rukwa kujiunga na
chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa ili kuwa na umoja na nguvu katika
kutafuta masoko ya mazao yao, kuachana na walanguzi, kulima kwa tija na
kuzalisha mazao bora kwa kupata pembejeo kwa wakati na hatimae kufanya
kazi kwa karibu na wataalamu wa kilimo waliomo ndani ya mkoa.
Amesema kuwa chama kikuu cha
Ushirika cha Mkoa Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU) ni chama kipya na
kinahitahi nguvu ya vyama vya ushirika vya mkoa mzima ili kiwe na
uongozi uliokamilika, kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza
kumnyanyua mkulima wa mkoa wa Rukwa kutoka alipo sasa na kuwa wakulima
wa hadhi ya kimataifa.
“Mkulima ana mahangaiko makubwa
sana, sasa huu ushirika ni chombo cha kumkomboa mkulima, ni chombo cha
kunyanyua uchumi wa mkulima, ni chombo cha kuikomboa Rukwa, ni chombo
cha kuikomboa nchi yetu ya Tanzania, nchi ambayo sasa inaelekea kwenye
uchumi wa kati wa viwanda, sasa ushirika ni kitovu cha uzalishaji n ani
kitovu cha viwanda, sasa kila tunachokifanya tuchote kwenye ngazi ya
mkulima, lazima tujue namba moja kwenye viwanda ni uzalishaji na
malighafi za kilimo zinatokana na wakulima, ni lazima azalishe na
akizalisha zaidi tutakuwa na viwanda endelevu kutokana na uzalishaji
mwingi” Alisisitiza
Ameongeza kuwa hali ya hewa ya
mkoa wa Rukwa ni sawa na hali ya hewa za mikoa yote ya nyanda za juu
kusini ambayo mikoa hiyo inaongoza kwa kulima matunda na mbogamboga na
hivyo kuwa na mazao mengi mbadala kuliko kutegemea mahindi ambapo soko
linaposhuka na wananchi wanakosa pa kukimbilia na hivyo kuwataka
wajitafakari kutoka katika kilimo cha kutegemea mahindi na hatimae
kuanza kulima mbogamboga na matunda ya kutosha kwaajili ya matumizi ya
wana-Rukwa ili kupunguza udumavu pamoja na kuuza nje ya mikoa na hatimae
nje ya nchi.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika
Mkutano wa Vyama vya ushirika Mkoani humo aliouitisha ili kuwatafutia
wanachama wapya chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa pamoja na kusikia
mipango yao waliyojiwekea kuanzia wa mawaka mmoja hadi miaka kumi katika
kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati chini ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli.
Akitoa taarifa fupi ya hali ya
vyama vya ushirika Kaimu Mrajisi vyama vya Ushirika wa mkoa wa mkoa wa
Rukwa Anosisye Mbetwa amesema kuwa miongoni mwa mafanikio ya mkoa ni
kuanzisha chama cha kikuu cha ushirika (UCU) ambacho kimesajiliwa tarehe
9.1.2019 kikiwa na wanachama 58 na kwa ujumla hadi kufikia tarhe
31.6.2019 mkoa umeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi
17,781,678,000/=.
“Vyama vya Ushirika 81 vimeweza
kukaguliwa na shirika la Ukaguzi la vyama vya Ushirika nchini (COASCO)
na kuhusu masoko kwa mwaka 2018/2019 soko la Serikali kwa maana ya NFRA
liliwezesha upatikanaji wa shilingi 3,010,467,520/= kwaajili ya ununuzi
wa mazao ya wakulima kupitia vyama vya Ushirika vya msingi,” Alisema.
Akielezea mpango wa Miaka 10 ya
Chama kikuu cha Ushirika Mkoani Rukwa Makamu Mwenyekiti wa UCU Gaspar
Chipeta amesema kuwa lengo kuu la chama hicho ni kuwaleta pamoja
wakulima wa mkoa wa huo, kuwa na sauti moja, kutambua mahitaji ya
pembejeo kwa kila mkulima kupitia vyama vya msingi pamoja na kutafuta
soko lenye bei nzuri ili kuweza kuinua uchumi wa wakulima.
“Mkakati mwingi ni kuhakikisha
ndani ya hii miaka kumi kuna matokeo ya uboreshwaji wa miundombinu
inayotumika katika kilimo, asilimia kubwa ya wakulima katika mkoa wa
Rukwa hawatumii miundombinu ya kisasa, kama ulivyosema awali kwamab
lazima twende kwenye kilimo cha kisasa, sisi kama chama kikuu tunataka
walau kila chama cha ushirika cha msingi, Kila AMCOS iweze kumiliki
walau Trekta ambalo litaweza kuwasaidia wakulima wa vyama hivyo,”
Alisema.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya
Sumbawanga Wakala wa Taifa wa Hiafadhi ya Chakula (NFRA) Abdillah
Nyangasa ametahadharisha wakulima wengi wamekuwa wakilima eneo kubwa
lakini mazao yanayopelekwa sokoni hayafanani na viwango na hivyo
kuwataka kuzingatia ubora wa mazao katika hatua ya mwisho ambayo
inapelekwa kwa mlaji, hali ambayo ipo katika mazao mengi yanayolimwa
katika Mkoa.
“ Eneo la Ubora baada ya mavuno ni
la msingi mno katika kupata soko zuri, wakati mwingine unaweza kuwa
umevuna vizuri lakini unaleta mahindi yako sokoni utaambiwa pepeta,
utaambiwa pembua mahindi yaliyooza, ondoa punji zilizoharibika na
wadudu, ile ni hatua ya ziada mabayo uneifanya mwenyewe kwenye ngazi ya
kaya na kwenye hatua ya chama cha msingi, tukazane kuhakikisha mazao
yetu tunayaandaa vizuri kwaajili ya soko ili kupunguza gharama zisizo za
lazima,” Alifafanua.
Mkoa wa Rukwa una jumla ya vyama
vya Ushirika 172, kati ya hivyo 87 ni vyama vya ushirika wa Akiba na
Mikopo (SACCOS), 74 ni vyama vya Mazao na Masoko (AMCOS), 4 vyama vya
Uvuvi, 3 vyama vya Wafugaji, 1 chama cha Wafuga Nyuki, 3 vyama vya wauza
Bidhaa/huduma na Chama Kikuu cha Ushirika kimoja vyenye jumla ya
wanachama 19,321.
No comments:
Post a Comment