Thursday, August 15, 2019

RAIS MAGUFULI: TUTAZIDI KUFUNGUA MILANGO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NA JAMHURI YA AFRIKA KUSINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kabla ya kuanza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipongezana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mara baada ya kubadilishana zawadi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MheshimiwaDkt. John Pombe Magufuli akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa pamoja  naujumbe wake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya AfrikaKusini Cyril Ramaphosa wakati wakizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mara baada ya kumaliza kikao chao na Waandishi wa Habari Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU
RAIS Dkt. John Magufuli amesema Tanzania itazidi kufungua milango ya ushirikiano na Jamhuri ya Afrika Kusini na kuwataka Wafanyabiashara na Wawekezaji wa nchi hizo kutumia fursa za vivutio mbalimbali vilivyopo ili kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa Mataifa hayo.
Akizungumza leo Alhamisi (Agosti 15, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais Magufuli alisema Tanzania na Afrika Kusini ni mataifa rafiki yenye historia ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aliongeza kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini ni miongoni mwa Mataifa yaliyopiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi katika Bara la Afrika, hivyo Tanzania itatumia fursa hiyo na mshirika wa karibu kwa ajili ya kupanua wigo wa sekta za kibiashara ikiwemo ununuzi na uuzaji wa bidhaa na mazao mbalimbali.
“Katika Nchi za SADC, mwaka 2018 Tanzania imeongoza katika ukanda wa SADC kwa thamani ya mauzo ya bidhaa zake Nchi ya Afrika Kusini iliyofikia thamani Dola Milioni 742.02, na biashara baina ya Mataifa haya ilifikia thamani ya Dola Bilioni 1.18 kutoka Dola Bilioni 1.11 mwaka 2017” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alitoa wito kwa Wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusni kuja kwa wingi nchini kwa ajili ya kuwekeza na kufanya biashara kwa kuwa Serikali imeendelea kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi ikiwemo ujenzi wa miundombionu ya uhakika, pamoja na uimarishaji wa mifumo ya kitaasisi katika usimamizi wa kodi na biashara.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Tanzania imejipanga kikamilifu katika kuimarisha mfumo imara wa uchumi wake ikiwemo kupitia ujenzi wa viwanda, ambayo ndiyo Dira na dhamira ya Serikali ya Awamu ya  Tanzania katika kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo aliwataka wawekezaji wa Afrika Kusini kuja nchini na kujenga viwand.
“Katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka tunatenga kiasi cha Tsh Bilioni 270 kwa ajili ya ununuzi wa madawa nje ya nchi, tunawaomba wawekezaji wa Afrika Kusini waje Tanzania wajenge viwanda vya madawa kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza gharama kubwa za uagizaji wa madawa kutoka nchi ya nchi” alisema Rais Magufuli.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Serikali imekusudia miundombinu ya usafiri wa reli Tazara ili kuweza kutumika na Wafanyabiashara wa Afrika Kusini kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na kutangaza fursa za vivutio vya utalii na fukwe za bahari zenye urefu wa takribani Kilometa 1400 zilizopo nchini.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema Tanzania ipo tayari kufanya biashara na Jamhuri ya Afrika Kusini ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo magari, ambayo Tanzania imekuwa ikiyanunua katika nchi za mbali, huku akitolea mfano wa pikipiki zinazotumika katika Mkutano wa 39 wa SADC zimenunuliwa kutoka nchini Afrika Kusini.
Kwa upande wake Rais Cyril Ramaphosa alisema ziara yake nchini Tanzania ni kielelezo cha kuendelea kuimarika kwa ushirikiano baina ya Mataifa hayo na kusema Serikali yake itaweka mazingira wezeshi kwa Wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kwenda nchini Afrika Kusini kufanya biashara na kutafuta fursa ya maeneo ya uwekezaji na biashara.
Aliongeza kuwa Serikali yake inatambua umuhimu wa sekta ya biashara na uwekezaji katika kukuza uchumi katika Nchi za SADC kupitia ajenda ya Maendeleo Endelevu ya jumuiya hiyo ya mwaka 2030 ambayo imedhamiria katika kujenga mazingira bora ya biashara katika Jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment