Monday, August 19, 2019

GAMBO ATAKA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZA MIPAKA KATI YA TANZANIA NA KENYA BADALA YA KUSHINDANA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akifungua kikao cha Uimarisha Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya leo tarehe 19 Agosti 2019 kinachoendelea mkoani Arusha. Wa tatu kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Hamdoun Mansoor.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu wakati wa ufunguzi wa kikao ha Uimarishaji mpaka kati ya Tanzania na Kenya kinachoendelea mkoani Arusha leo tarehe 19 Agosti 2019. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Ujumbe wa Kenya Justa Nkoroi.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akitoka katika kikao cha Uimarishaji mpaka kati ya Tanzania na Kenya kinachoendelea mkoani Arusha baada ya kukifungua leo tarehe 19 Agosti 2019. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu na wa pili kushoto ni Mkuu wa Ujumbe wa Kenya Justa Nkoroi.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akiwa katika picha ya pamoja kati ya ujumbe wa Tanzania na Kenya unaoshiriki kikao cha Uimarishaji mpaka kati ya nchi hizo mbili. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

………………………..
Na Munir Shemweta, WANNM ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewataka wajumbe wanaoshiriki kikao cha Uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya kutumia kikao hicho kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za mipaka badala ya kushindana.
Mrisho Gambo alitoa kauli hiyo leo tarehe 19 Agosti 2019 wakati wa kufungua kikao cha cha muendelezo wa Uimarishaji mipaka ya kimataifa baina ya Tanzania na Kenya kinachoendelea jijini Arusha.
Alisema, anafarijika sana kuona utatuzi wa changamoto za mipaka ya kimataifa kati ya Kenya na Tanzania unafanywa na nchi husika bila kushirikisha mataifa ya nje na kusema kuwa hiyo inaonesha ni jinsi gani nchi hizo zinavyoweza  kukaa pamoja kwa kujiamini na kupata ufumbuzi wa masuala yake.
Aliwataka wajumbe wa kikao cha nchi hizo mbili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mipaka ya kimataifa kati yao kwa kukubaliana na kuzingatia  tamaduni za nchi hizo sambamba na  miongozo ya viongozi wa nchi husika.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa wa Arusha aliwataka washiriki kudumisha pia mahusiano ya kijamii wakati wa majadiliano yao kwa kuwa wananchi wanaoishi  mipakani  wana mahusiano mazuri ya kindugu na kusisitiza kuwa hali hiyo itadumisha umoja na mshikamano uliopo kati ya nchi hizo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu alisema kikao hicho cha siku tano ni muendelezo wa vikao vya uimarishaji mipaka ya kimataifa katika maeneo mbalimbali ya mipakani ikiwa na lengo la kuondoa changamoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika (AU).
Kwa mujibu wa Kabundugulu, Kikao hicho kitapokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha mpaka cha kilomita 128 kutoka eneo la Ziwa Natron hadi Namanga mkoani Arusha ambapo lengo ni kuimarisha mpaka huo hadi Tarakea mkoani Kilimanjaro na baadaye Jasini mkoani Tanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Ujumbe kutoka Kenya Justa Nkoroi alisema kikao hicho ni muhimu kwa mustakabali wa nchi za Tanzania na Kenya katika kuangalia changamoto za alama za mipaka ya kimataifa iliyowekwa wakati wa ukoloni na kubainisha kuwa ana imani kikao hicho  kutatatua changamoto zilizopo na hatimaye kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa na Umoja wa Afrika mwaka 2022.
Tayari jumla ya Kilomita 172 kutoka ziwa Victoria hadi Loliondo mkoani Arusha zimeimarishwa kwa kuwekwa alama (Pillars) za mipaka kati ya Tanzania na Kenya kwa umbali wa mita zisizozidi mita 100 ili zionekanane kwa urahisi na wananchi wanaoendesha shughuli zao katika maeneo ya mipakani.

No comments:

Post a Comment