**********
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah awasake
na kuwatia mbaroni watu waliohusika na wizi wa tani tano za nondo na
kisha wakatoroka.
Alitoa agizo hilo jana jioni,
(Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza na wafanyakazi na wananchi
mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya kimataifa
ya Moshi, katika kata ya Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani
Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi za siku nne, alisema mradi huo ni
maalum kwani uko miongoni mwa miradi ambayo Serikali imekuwa ikiweka
utaratibu wa kupelekea fedha kwenye miradi iliyotengwa na Halmashauri.
“Serikali imetenga kiasi cha
shilingi bilioni 9 za kuanzia mradi huu lakini inasikitisha kuona kwamba
wanaMoshi mnahujumu kwa kuiba vifaa vya ujenzi. Ninazo taaarifa kuwa
hapa zimeibiwa tani tano za nondo na zimeshakamatwa.”
“Ni aibu, ni aibu kwa
wana-Moshi. Ninyi wenyewe mnauhujumu huu mradi. Manispaa iweke utaratibu
wa ulinzi ili vifaa vingine visipotee zaidi. Mkuu wa Wilaya chukua
hatua ya kuwafuatilia wote waliohusika,” alisema.
Kupitia maswali aliyouliza,
Waziri Mkuu alibaini kuwa walinzi wawili waliokuwepo siku ya tukio
walitoroka ndipo akaamua kumwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa, awasake na
kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Ujenzi wa stendi hiyo kubwa
unafanywa na mkandarasi mkuu ambayo ni kampuni ya CRJE ya China
akishirikiana na wakandarasi wasaidizi watano na unatarajiwa kukamilika
Januari 2021. Hadi kukamilika, ujenzi huo unatarajiwa kugharimu sh.
bilioni 28.8.
Ikikamilika, stendi hiyo
ambayo itakuwa na ofisi, maduka, migahawa na hoteli, itakuwa na uwezo wa
kuhudumia mabasi 300 kwa siku ambayo yataingia na kutoka. Kati ya hayo,
mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja. Pia kutakuwa na maegesho
ya ya magari binafsi 218, teksi 34 na bajaji na bodaboda 20.
Wakati huohuo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amethibitisha kukamatwa kwa
watu watano ambao wanatuhumiwa kuhusika na wizi wa tani tano za nondo
katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo lililopo Ngangamfumuni.
“Hawa watu tumewakamata jana
jioni, na kati ya walinzi waliotoroka, tumemkamata mmoja wao tayari
akiwemo mkazi wa Rau, Daudi Audifasi mwenye miaka 48 ambaye anadaiwa
kutoboa ukuta wa uzio kwa chini, na kukutwa na nondo nyumbani kwake
ambako ni mita 10 kutoka eneo la tukio.”
Amesema tukio hilo, lilitokea
Julai 6, mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi ambapo walinzi wa eneo hilo
ambao ni Maxshield company walitoroka baada ya tukio hilo. Kamanda Issah
alithibitisha kwamba nondo hizo zimekamatwa na ziko polisi.
No comments:
Post a Comment