Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali, akizungumza na wananchi na
waumini wa dini, kwenye maadhimisho ya miaka 80 ya kanisa hilo, Julai
21.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea ngao
kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli, kutoka kwa Askofu Mkuu wa Kanisa
la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali, kwenye
maadhimisho ya miaka 80 ya kanisa hilo, yaliyofanyika katika uwanja wa
Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Julai 21.2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
***********
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God kwa kuthamini na
kutambua kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.
“Baba Askofu Mtokambali
umenifurahisha kwa takwimu ulizozitaja hapa za miradi mikubwa ambayo
inatekelezwa na Serikali hii. Kuna wengine hawapendi kusikia mambo kama
haya, hongera sana,” amesema.
Ametoa pongezi hizo leo mchana
(Jumapili, Julai 21, 2019) wakati akizungumza na maelfu ya waumini wa
kanisa hilo katika maadhimisho ya miaka 80 ya TAG hapa nchini
yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni
rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, amesema ameguswa na jinsi
kanisa hilo linavyomtambua Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake na
kuthamini juhudi za Serikali.
“Serikali hii imedhamiria
kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini zenu, rangi wala itikadi za
kisiasa. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano
itaendelea kumtegemea Mungu pasipo shaka yoyote.”
Pia amewapongeza viongozi wa
kanisa hilo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka
80. “Pia nikupongeze Baba Askofu kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji
kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari hapa Arusha. Natambua kwamba
ulishachangia mifuko mingine 500, asante sana.”
Alilishukuru kanisa hilo kwa
kuendesha maombi maalum kwa ajili ya Taifa yaliyoongozwa na Mchg. Titus
Mkama. “Niliguswa sana wakati maombi ya Taifa yalipokuwa yakiendelea.
Mchungaji aligusia masuala ya muhimu kwa Taifa hili.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na maelfu ya washirika waliohudhuria maadhimisho hayo, Askofu
Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali alisema anamshukuru Mheshimiwa
Rais Dkt. Magufuli kwa kulipenda na kulijali kanisa hilo.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa
miradi mikubwa ya maendeleo anayoisimamia kama vile umeme wa Stiegler’s
Gorge, reli ya SGR, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali mpya 67 za
wilaya, ujenzi wa vituo vya afya 370 na ununuzi wa dawa za hospitali.
“Nina umri wa kutosha lakini
katika miaka yangu yote hii, sijawahi kuona hospitali 67 zikijengwa kwa
pamoja. Tena, mwaka huu wa fedha mmetenga hela kwa ajili ya ujenzi wa
hospitali nyingine 27. Hongera sana kwa ujasiri huo,” alisema Dkt.
Mtokambali.
Maadhimisho ya miaka 80 ya TAG yameenda sambamba na hitimisho la miaka 10 ya Mpango Mkakati wa mavuno.
No comments:
Post a Comment