WAZIRI MKUU AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU WA VIET NAM
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza
na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung, katika mazungumzo ya
faragha yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es
salaam, Julai 12, 2019
………………
*Awakaribisha Waviet Nam waje kuwekeza katika bandari, usafiri wa anga na kilimo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekuna na
kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Viet Nam, Trinh Dinh Dung na
amewakaribisha wawekezaji kutoka Viet Nam waje kuwekeza kwenye maeneo
mbalimbali yakiwemo ya mipango miji, madini, bandari, usafiri wa anga,
ufundi stadi, kilimo pamoja na uvuvi.
Amesema kuwa anatambua kwamba nchi ya
Viet Nam inafanya vema katika suala la mazao ya kilimo kwa kuongeza tija
kwenye mazao hayo na kukifanya kilimo kuwa cha biashara, hivyo
amezialika kampuni za Viet Nam zenye teknolojia mahsusi katika maeneo
tajwa ili kushirikiana na Tanzania katika mikakati yake ya kuendeleza
kilimo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa,
Julai 12, 2019) wakati wa mkutano wake na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Kisoshalisti ya Viet Nam , ambapo ametumia fursa hiyo kumuhakikishia
kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Viet Nam kwa
manufaa ya watu wa nchi mbili hizo.
Amesema uwepo wa kampuni ya Viettel PLC
(Halotel) ya kutoka nchini Viet Nam ni ishara tosha ya imani ya
uwekezaji iliyopo kwa wawakilishi wa Viet Nam. “Nawakaribisha sana
wawekezaji kutoka Viet Nam kuja kuwekeza Tanzania kwani kwa kufanya
hivyo hawatojutia uamuzi wao wa kuwekeza Tanzania.”
Waziri Mkuu amesema Viet Nam imeendelea
kuwa mshirika muhimu wa kiuchumi kwa Tanzania, hivyo ametumia fursa hiyo
kuishukuru Serikali ya Viet Nam kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya
Tanzania katika jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo.
“Kwa mfano, kampuni ya mawasiliano ya
Viettel PLC (maarufu kama Halotel) ambayo imewekeza nchini tangu mwaka
2014 inafanya vizuri katika sekta ya mawasiliano. Kampuni hiyo,
imewezesha mawasiliano ya simu kuwafikia Watanzania wengi hususan wale
waishio vijijini.”
Waziri Mkuu amesema kampuni hiyo ya
Halotel imeweza kuzalisha ajira takriban 1,600 za moja kwa moja kwa
wazawa na ajira takriban 100,000 zisizokuwa za moja kwa moja hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka 2018;
Amesema lengo la Serikali ya Tanzania ni
kuendelea kushirikiana na Serikali ya Viet Nam katika masuala ya
mawasiliano na masuala mengine ikiwemo biashara na uendelezaji na masoko
ya mazao ya kilimo hususan korosho, kahawa, kilimo mseto cha mpunga na
uvuvi wa samaki ambako Viet Nam inafanya vizuri zaidi.
Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii,
Waziri Mkuu amesema Tanzania ni nchi nzuri, watu wake ni wakarimu na pia
imebarikiwa vivutio vingi vya utalii. Hivyo, amezikaribisha kampuni za
Viet Nam kuja kuwekeza katika sekta ya utalii na utamaduni nchini.
“Halikadhalika, sina shaka kwamba wengi
wenu mmewahi kusikia kuhusu Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro,
pamoja na Mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Hivyo ni baadhi tu ya
vivutio vingi vya utalii tulivyojaliwa kuwa navyo nchini mwetu.”
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Viet Nam, Trinh Dinh Dung
ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushgirikiano na kwamba ameomba
ushirikiano huo uimarishwe kupitia ziara za viongozi wa wakuu wa nchi
mbili hizo.
Naibu Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya
Kisoshalisti ya Viet Nam, amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba Serikali ya
Viet Nam itazidi kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania
hususani katika sekta za kilimo, biasdhara na uvuvi.
Kadhalika kiongozi huyo amesema kuwa nchi
ya Viet Nam iko tayari kununua mazao mbalimbali ya kutoka nchini
Tanzania yakiwemo ya korosho na pamba. Amesema lengo la Serikali yao ni
kuhakikisha kwamba biashara kati ya Tanzania na Viet Nam inafikia dola
bilioni moja ifikapo 2020.
No comments:
Post a Comment