Friday, July 12, 2019

Mgogoro Baina ya Wazee wa Kimila na Chuo cha Ufundi Arusha Watatuliwa

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi akisistiza jambo wakati wa kikao cha usuhushi  baina ya Wazee wa kimila wa kimasai na uongozi wa chuo cha Ufundi Arusha kuhusu eneo la kimila lililopo ndani ya chuo hicho leo Jijini Arusha.

Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi akiwa amemwakilisha  Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde (kushoto) akifafanua jambo  katika kikao cha usuluhishi baina ya Wazee wa kimila wa kimasai na uongozi wa chuo cha Ufundi Arusha kuhusu eneo la kimila lililopo ndani ya chuo hicho, kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi.

Mwenyekiti wa Wazee wa Kimila wa Kimasai Bw. Isack Lekisongo akitoa neno la shukurani  katika kikao cha usuluhishi baina ya Wazee wa kimila wa kimasai na uongozi wa chuo cha Ufundi Arusha kuhusu eneo la kimila lililopo ndani ya chuo hicho leo Jijini Arusha.

Wajumbe wakisikiliza na kufuatilia kwa makini maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi (hawapo katika picha) wakati wa  kikao cha usuluhishi baina ya Wazee wa kimila wa kimasai na uongozi wa chuo cha Ufundi Arusha kuhusu eneo la kimila lililopo ndani ya chuo hicho leo Jijini Arusha.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi (kulia) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Wazee wa Kimila wa Kimasai Bw. Isack Lekisongo (kushoto) wakati wa  kikao cha usuluhishi baina ya Wazee wa kimila wa kimasai na uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha kuhusu eneo la kimila lililopo ndani ya chuo hicho leo Jijini Arusha

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi( wa pili kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa kikao cha usuluhishi wa eneo la kimila lililopo katika Chuo Cha Ufundi Arusha mara baada ya kufikia makubaliano leo Jijini Arusha.( Picha na Lorietha Laurence-WHUSM, ARUSHA)

………………….

Na Lorietha Laurence-WHUSM,ARUSHA

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamefanikiwa kutatua mgogoro  wa muda mrefu baina ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Wazee wa kimila wa Kimasai kuhusu umiliki wa eneo la kimila lilipo ndani ya chuo hicho.

Akiongea katika kikao  kilichofanyika leo Jijini Arusha Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Bi. Susan Mlawi ameueleza kuwa ni muhimu kwa uongozi wa chuo pamoja na uongozi wa wazee wa kimila kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza makubaliano yaliyoafikiwa katika kikao cha awali kilichofanyika tarehe 17 Mei 2019.

Moja ya makubaliano hayo ni pamoja na uongozi wa chuo kuongeza eneo  hilo la kimila la Wazee wa Kimasai kutoka meta mraba 1,118.12 hadi kufikia meta mraba 1,464.92 ili kuwapa nafasi ya kufanya shughuli hizo za kimila.

“Kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza na kudumisha mila katika jamii yetu ya kitanzania sisi viongozi wa serikali tumeona umuhimu wa chuo kuongeza eneo hili  ili muweze kupata nafasi ya kufanya shughuli za kimila “ alisema Bibi. Susan Mlawi

Aidha aliongeza wa kueleza kuwa mbali na kuongezewa eneo, kikao  kimekubaliana na kuruhusu uongozi wa jamii ya kimasai kumalizia ujenzi wa jengo lililopo katika eneo hilo pamoja na kujenga vyoo vya kisasa.

Vilevile kikao hicho  kilisisitiza kuwa eneo hilo litumike kwa masuala ya kimila tu na si vinginevyo huku umiliki wa ardhi ya eneo ukiendelea kuwa chini ya uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha.

Pia kikao kiliazimia kuwa viongozi hao wa kimila wataendelea kufuata utaratibu wa kuomba kibali kutoka katika uongozi wa chuo ili kuweza kuingia katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali za kimila.

Naye Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde  amewataka viongozi hao wa kimila kuzingatia makubaliano hayo na kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa uongozi wa Chuo.

“Makubaliano haya ni mazuri yenya lengo la kujenga mahusiano mema baina ya Serikali na wananchi wake hivyo ni muhimu kuzingatia yale yote tuliyokubalina hapa kwa maendeleo na ustawi mzuri wa nchi yetu” alisema Dkt. Noel Mbonde.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazee wa Kimila wa Kimasai Bw. Isack Lekisongo ameishukuru  serikali pamoja viongozi walioshiriki kufikia muafaka wa kuutatua mgogoro huo wa mrefu na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu katika kutekeleza  shughuli zao za kimila.

No comments:

Post a Comment